Kimataifa

Taharuki na hofu Cameroon kinara wa upinzani akifariki kizuizini

December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

YAOUNDE, CAMEROON

KIONGOZI wa Upinzani Anicet Ekane aliaga dunia kizuizini mnamo Jumatatu usiku.

Familia ya Ekane, 74 na wakili wake, walithibitisha kifo chake huku mauti yake yakizua taharuki kubwa ya kisiasa nchini humo.

Ekane, Kiongozi wa Chama cha MANIDEM, alikamatwa mnamo Oktoba 24 baada ya maandamano kutanda nchini humo kufuatia kutangazwa kwa ushindi wa Rais Paul Biya.

Chama chake kilisema kuwa alikuwa ametekwa nyara na wanajeshi wa Cameroon.

Katika uchaguzi huo, Ekane alimuunga mkono mwaniaji wa upinzani Issa Tchiroma Bakary ambaye amekimbilia uhamishoni kuhepa kunyakwa na serikali.

Alikuwa akizuiliwa kutokana na mashtaka ya uchochezi na kutoa wito kwa raia wakatae serikali ya Biya.

Kifo chake kinaonekana kimeongeza taharuki nchini humo hasa baada ya takwimu kutolewa kuwa raia 48 waliuawa wakati wa maandamano dhidi ya Rais Biya.

Rais huyo ndiye mkongwe zaidi akiwa na umri wa miaka 92, akiwa ameongoza Cameroon tangu 1982.

Siku chache alipotembelewa na wakili wake pamoja na wanafamilia, Ekale hakuweza kuzungumza kwa mujibu wa wakili wake Ngouana Ulrich Juvenal.

Dadake Mariane Simon-Ekane alithibitisha kifo hicho kupitia ujumbe aliouweka kwenye Facebook.

Naye Wizara ya Ulinzi ya Cameroon ilisema Jumatatu kuwa ilikuwa ikiendeleza uchunguzi kuhusu mauti hayo.

Jeshi lilisema tu kiongozi huyo alifariki katika kituo cha matibabu cha jeshi na kusisitiza kuwa aliaga kutokana na maradhi ya moyo.

Chama chake kupitia taarifa mnamo Novemba 21, kilisema kuwa vifaa vya kimatibabu vya kiongozi huyo ambavyo alivihitaji vilifungiwa kwenye gari lake ambalo lilitwaliwa na vyombo vya usalama jijini Douala.

Chama hicho kilishutumu kamanda wa kituo husika kwa kuzima majaribio ya mawakili wake kupata vifaa hivyo vya kimatibabu.

Chama kiliongeza kuwa serikali ndiyo ilisababisha mauko ya Ekane kwa kumzuilia licha ya hali yake mbaya kiafya na ikakataa asitibiwe kabisa.

Ekane alikuwa akizuiliwa na mwanachama wa chama chake, Florence Aimee Titcho pamoja na wafuasi wengine Issa Tchiroma Bakary.

Upinzani ulikemea kuendelea kuzuiliwa kwao huku ukishikilia kuwa Tchiroma alishinda uchaguzi huo.

Tchiroma mwenyewe yupo uhamishoni Gambia ambako amepewa hifadhi kwa msingi wa msaada wa kibinadamu kulingana na serikali ya Gambia.

Rais Biya alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 56 dhidi ya 38 ya kura za Tchiroma na ataongoza Cameroon kwa kipindi kingine cha miaka saba zaidi, akitinga miaka 99 wakati ambapo utawala wake utakuwa ukitamatika ikiwa bado atakuwa hai