Taharuki Uganda baada ya Ebola kuua mtu wa pili
Na LILIAN NAMAGEMBE, MWANDISHI WA DAILY MONITOR
UGONJWA hatari wa Ebola unazidi kusababisha maafa nchini Uganda baada ya mtu wa pili kufariki jana huku maafisa wa afya wakifanya kila wawezalo kuzuia kuenea kwake.
Ripoti zilisema kuwa nyanyake mvulana aliyefariki Jumatano ndiye mtu wa hivi punde kufariki kutoka na virusi vya ugonjwa huo uliosambaa kutoka taifa jirani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Nyanya huyo alifariki usiku wa kuamkia jana katika Hospitali Kuu ya Bwera ambako kitengo maalum cha kuwatibu wagonjwa wa Ebola kilianzishwa baada ya mvulana huyo mwenye umri wa miaka mitano kufariki katika eneo la Kesese Magharibi mwa Uganda.
“Atazikwa kesho na maafisa wetu baada ya wao kutambua eneo maalum,” afisa mmoja wa Wizara ya Afya ambaye ni miongoni mwa wale walioenda Kasese, jana Alhamisi, aliambia gazeti la Daily Monitor.
Hata hivyo, afisa huyo alidinda kutajwa jina kwa sababu haruhusiwi kuongea na wanahabari.
Msemaji wa Wizara ya Afya Bw Emmanuel Ainebyoona alikataa kuzungumzia suala hilo huku Waziri wa Afya Dkt June Ruth Aceng akikataa kujibu simu tulipotaka kuthibitisha kisa hicho.
Mlipuko wa Ebola umesababisha mauaji ya watu kadha Mashariki mwa DRC katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Kisa cha ugonjwa huo kilithibitishwa kwa mara ya kwanza nchini Uganda katika wilaya ya Kesese inayopakana na nchi hiyo.
Kisa hicho kilikuwa ni cha mvulana mwenye umri wa miaka mitano aliyepatina na virusi vinavyosababisha Ebola. Mvulana huyo alifariki mnamo Jumatano akipokea matibabu maalum katika kituo maalum cha Ebola mjini Kesese.
Wengine waliopatikana na virusi vya ugonjwa huo hatari ni kakake marehemu ambaye amelazwa katika wadi maalum ya kutibu Ebola katika Hospitali Kuu ya Bwera.
Wengine saba
Mnamo Jumatano Waziri wa Afya Dkt Aceng alifichua kuwa kuna watu wengine saba wanaoshukiwa kuambukizwa ugonjwa huo hatari.
Miongoni mwao ni wanaume wawili, wanawake wawili na mtoto mwenye umri wa miezi sita; wote ambao inasemekana walikuwa wamesafiri kutoka nchini DRC. Walikuwa wamekuja kuhudhuria nchini Uganda kabla ya kuanza kuugua.
Wote hao wanatibiwa katika kitengo maalum cha kilichoanzishwa maalumu kutibu Ebola katika Hospitali Kuu ya Bwera.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) jumla ya watu 1,390 wamefariki kutokana na mara ya Ebola kufikia sasa. Watu wengine 2,062 wanaendelea kutibiwa katika vituo mbalimbali vya kiafya nchini humo.
Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini Uganda limetangaza kuwa linasaidiana na serikali ya Uganda kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo hatari.
“Hili ni tukio la kutamausha lakini tumekuwa tukijiandaa kwa hali kama hii kwa miezi kadhaa ikizingatiwa kuwa Uganda inapakana na mashariki mwa DRC ambako ugonjwa huo umesababisha maafa makubwa,” Katibu Mkuu wa shirika hilo Robert Kwesiga akasema kwenye taarifa mnamo Jumatano.