Kimataifa

TANZIA: Oliver Mtukudzi alivyotambulika kimataifa

January 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

CHARLES WASONGA Na MASHIRIKA

MWANAMUZIKI maarufu nchini Zimbabwe, na mwenye sifa kimataifa, Oliver Mtukudzi alifariki Jumatano baada ya kuugua ugonjwa wa kisukari, vyombo vya habari nchini Zimbabwe vimeripoti.

Mtukudzi, almaarufu Tuku, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 66 amevuma katika ulingo wa muziki kwa miongo minne amefumua jumla ya albamu 66.

Mwanamuziki huyo alifariki katika hospitali moja jijini Harare, kulingana na ripoti katika gazeti la Herald linalomilikiwa na serikali.

Kufikia Jumatano jioni hakuna habari zozote ambazo zilikuwa zimetolewa kuhusu kifo chake na familia yake wala promota wake..

Mtukudzi alianza kuimba mnamo 1977 akishirikiana na mwanamuziki mwingine kwa jina Thomas Mapfumo ambaye alitunga nyimbo zenye maudhui ya kupinga maovu katika jamii.

Kupitia sauti yake mzuri, Mtukudzi aliibuka kuwa mwanamuziki aliyetambuliwa na kuhusudiwa zaidi nchini Zimbabwe na katika mataifa ya bara Afrika.

Mwamuziki huyo alijiepusha na maudhui ya kisiasa katika nyimbo zake, ambazo kimsingi ziliangazia masuala ambayo huathiri maisha ya wanadamu maishani.

Lakini mnamo 2001, kibao chake kwa jina “Wasakara” (kwa maana wewe ni mzee) kutoka kwa albamu yake “Bvuma” (Uvumilivu) kilifasiriwa na wengi kama kilichomlenga rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe. Wakati huo Mzee Mugabe alikuwa ameshinda uchaguzi wa urais katika kupitia njia ambayo iliibua utata mkubwa.

Muziki wa Mtukudzi unaenziwa na watu wa vizazi mbalimbali. Na katika miaka ya nyuma alichomoa vibao kadhaa akishirikiana na wanamuziki chipukizi, baadhi yao wakiwa wale ambayo alisaidia kukuza talanta zao katika kituo chake cha sanaa kilichoko katika eneo la Norton, kitongojini mwa jiji la Harare.

Amewahi kurekodi nyimbo kwa ushirikiano na kundi la Black Mambazo kutoka Afrika Kusini na marehemu Hugh Masekela.

Masekela alikuwa gwiji wa uchezaji tarumbeta na muziki chapa Jazz nchini Afrika Kusini, huku akitumia muziki wake kuendeleza mapambano dhidi ya sera ya ubaguzi wa rangi.