Kimataifa

Tetemeko kubwa la ardhi lasababisha hofu ya tsumani nchi kadhaa Bahari ya Pacific

Na REUTERS, BENSON MATHEKA July 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TETEMEKO kubwa la ardhi la kipimo cha 8.8 lilitokea karibu na Penisula ya Kamchatka mashariki mwa Urusi Jumatano, na kusababisha tsunami ya hadi urefu wa mita 4 (futi 13), kuharibu majengo na kuchochea tahadhari na uhamishaji wa watu kutoka maeneo mbalimbali ya Bahari ya Pacific.

Watu kadhaa walijeruhiwa katika eneo la mbali la Kamchatka, huku watu katika sehemu kubwa ya pwani ya mashariki ya Japani – ambayo iliharibiwa vibaya na tetemeko na tsunami mwaka wa 2011 – wakiamriwa kuhama.

“Tetemeko la leo ni kubwa sana na ni lenye nguvu zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa,” alisema Gavana wa Kamchatka, Vladimir Solodov, katika video aliyochapisha kwenye mtandao wa Telegram.

Tsunami yenye urefu wa kati ya mita 3 hadi 4 ilirekodiwa katika maeneo ya Kamchatka, kwa mujibu wa waziri wa masuala ya dharura wa eneo hilo, Sergei Lebedev, ambaye aliwataka watu waepuke maeneo ya pwani.

Taasisi ya Jiolojia ya Amerika (USGS) ilisema tetemeko hilo lilikuwa la kina kifupi – kilomita 19.3 (maili 12) chini ya ardhi – na lilikuwa umbali wa kilomita 119 (maili 74) mashariki-kusini mwa jiji la Petropavlovsk-Kamchatsky lenye watu 165,000.

USGS iliongeza ukubwa wa tetemeko kutoka kipimo cha 8.0 hadi 8.8, na baadaye iliripoti tetemeko jingine dogo la kipimo cha 6.9.

Shirika la hali ya hewa Japan liliongeza kiwango cha tahadhari yake, likisema kuwa linatarajia mawimbi ya tsunami ya hadi mita 3 kufikia maeneo ya pwani kuanzia asubuhi kwa saa za eneo hilo.

Shirika la utangazaji la umma NHK liliripoti kuwa serikali ilikuwa imetoa amri ya watu kuhama baadhi ya maeneo.

“Tafadhali hameni mara moja. Ikiwezekana, elekeenu maeneo ya juu au mbali na pwani haraka iwezekanavyo,” alionya mtangazaji wa NHK.

Wafanyakazi wa viwandani na wakazi katika kisiwa cha Hokkaido, kaskazini mwa Japani, walihamia kwenye vilima vinavyoangalia bahari, kama inavyoonyeshwa kwenye video ya runinga ya TBS.

Mfumo wa Amerika wa Tahadhari ya Tsunami pia ulitoa onyo kuhusu “mawimbi hatari ya tsunami” ndani ya saa tatu zijazo.

Mawimbi yanayozidi mita 3 yanaweza kufika baadhi ya fukwe za Urusi huku mawimbi ya mita 1 hadi 3 yakitarajiwa Japan, Hawaii, Chile na Visiwa vya Solomon.

Mawimbi madogo zaidi yanaweza kufika kwenye fukwe nyingi za Pacific, zikiwemo zile za pwani ya magharibi ya Amerika.

Hawaii iliamuru watu kuhama kutoka baadhi ya maeneo ya pwani.

“Chukua Hatua! Mawimbi ya tsunami yanayoweza kuharibu yanatarajiwa,” ilisema Idara ya Usimamizi wa Dharura ya Honolulu kwenye mtandao wa X.

Onyo hilo lilihimiza wakazi wa maeneo ya chini kuhama kwenda maeneo ya juu au hadi ghorofa ya nne ya jengo.