Kimataifa

Theresa May kukutana na Rais Kenyatta Ikulu ya Nairobi Alhamisi

August 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA PETER MBURU

WAZIRI Mkuu wa Uingereza Theresa May atafanya ziara yake ya kwanza bara la Afrika kama waziri mkuu wiki hii, katika matembezi yatakayohusisha nchi tatu.

Akiwa pamoja na mawaziri kadhaa na wawakilishi wa kibiashara, Bi May atazuru Kenya, Afrika Kusini na Nigeria katika ziara hiyo ya siku tatu, zikasema ripoti Jumatatu.

Atakuwa waziri mkuu wa kwanza kuzuru Kenya tangu wakati wa Margaret Thatcher, 1988.

“Tunapojiandaa kuondoka kutoka Umoja wa Ulaya (EU), huu ndio wakati wa kuzidisha ushirikiano na washirika wengine wa kidunia. Afrika iko katika nafasi nzuri ya kubadili dunia kiuchumi,” akasema Bi May katika habari hiyo.

“Ziara hii itakuwa fursa ya kipekee kwa Uingereza kuelezea maono yetu na kushirikianakwa karibu.”

Jumanne, watazuru jiji la Cape town ambapo Bi May atakutana na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, pamoja na viongozi wa kibiashara na vijana.

Aidha, waziri huyo mkuu anatarajiwa kutembea kisiwa cha Robben ambapo Rais Nelson Mandela alifungwa kwa miongo ili kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwake.

Jumatano ataelekea Nigeria ambapo atakutana na Rais Muhammadu Buhari jiji kuu la Abuja pamoja na wadhulumiwa wa mateso ya kisasa katika jiji la Lagos.

Alhamisi atafungia ziara yake nchimi Kenya ambapo atafanya kikao na Rais Uhuru Kenyatta, baada ya Bw Kenyatta kutoka Marekani ambapo yuko sasa.

Bi May kisha anatarajiwa kushuhudia mafunzo ya kijeshi ya vikosi vya Uingereza, azuru shule ya kibiashara kabla ya kushiriki mlo wa chajio utakaoandaliwa na Rais Kenyatta.