Kimataifa

Trump aanza kuwahamisha raia Wazungu kutoka Afrika Kusini kuwapa makao Amerika

Na MASHIRIKA May 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

PRETORIA, AFRIKA KUSINI

AFRIKA Kusini imekosoa Amerika huku ripoti zikiibuka na kuashiria kuwa Washington itawapokea raia wa Afrika Kusini wenye asili ya Amerika, Afrikaners, kama wahamiaji kuanzia wiki hii.

Nakala iliyoonekana na vyombo vya habari inataja mchakato huo wa uhamishaji kama “uliopewa kipaumbele” na serikali ya Rais Donald Trump, lakini ikulu ya White House haijathibitisha wakati.

Kwenye taarifa iliyochapishwa Ijumaa, wizara ya uhamiaji ilitaja hatua hiyo kama “inayochochewa kisiasa” na inayokusudiwa kudunisha “demokrasia ya kikatiba” nchini.

Februari, Trump aliwataja wanajamii wa Afrikaners kama waathiriwa wa “ubaguzi wa rangi” katika amri ya rais, na kuanzisha uwezekano wa kuwapa makao Amerika.

Serikali ilisema haitawazuia kuondoka waliochaguliwa kwa mpango huo wa makao, lakini ikasema imeitaka Amerika kuwahakikishia kwamba walioteuliwa wamepigwa msasa kikamilifu na hawana kesi zozote za uhalifu.

Aidha, taarifa ilisema madai ya kuwabagua wazungu walio wachache nchini hayana mashiko na kuwa takwimu za uhalifu hazijaashiria kuwa kundi lolote la watu wa asili fulani wamelengwa kwenye mashambulizi ya uhalifu mashambani.

Baadhi ya makundi yanayowakilisha haki za wakulima wazungu yamesema wanauawa kimaksudi kwa sababu ya asili yao.

Msemaji wa Wizara ya Uhamiaji Amerika alisema wanawahoji watu wanaotaka kuhamia Amerika na kuwapa umuhimu watu wa “Afrikaners” kutoka nchini Afrika Kusini ambao ni wahasiriwa wa ubaguzi usio wa haki kuhusu asili yao.

Serikali ya Trump vilevile imeshutumu Afrika Kusini kwa kuteka ardhi kutoka kwa wakulima wazungu bila kuwafidia, dai ambalo Pretoria imekanusha mara kwa mara.