Trump abadili nia ya kumrusha raia wa China nchini Uganda
WASHINGTON DC, AMERIKA
AMERIKA mnamo Ijumaa ilikatiza juhudi zake za kumrejesha kimabavu nchini Uganda raia wa China aliyesaidia kunakili dhuluma zinazodaiwa kutekelezwa na Beijing dhidi ya Waislamu wa Uyghur, wakili wa mwanamume huyo alieleza Reuters.
Guan Heng, mwanahabari mwenye asili ya China, alikimbilia Amerika mnamo 2021 baada ya kurekodi video ya kinachodaiwa kuwa kambi za kuwapakia mateka katika eneo la Xinjiang, China Magharibi.
Aliachilia video hiyo baada ya kuwasili Amerika ambapo alituma maombi ya kupatiwa hifadhi.
Guan alizuiliwa Agosti na idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Ushuru wa Forodha (ICE) kwa kuingia kimagendo taifa hilo, sehemu ya msako mkali unaoendeshwa na Rais Donald Trump dhidi ya wahamiaji.
Angali kizuizini katika jiji la New York. Kuzuiliwa kwake na tishio la kurushwa Uganda kumezua utata, hasa ikizingatiwa alisaidia kurekodi dhuluma zilizofanyika China ambazo serikali ya Amerika wakati wa hatamu ya kwanza ya Trump ilitaja kuwa “mauaji ya halaiki.”
Wafuasi na wakili wake wanasema Guan alikabiliwa na mateso waziwazi ikiwa atatoswa Uganda.
Taifa hilo la Afrika Mashariki, ambapo Beijing ina umaarufu kwa kiasi fulani kisiasa na kiuchumi, mwaka huu liliingia kwenye mkataba na Amerika kuwachukua raia kutoka mataifa maskini.
Chini ya sera za Wizara ya Usalama wa ndani (DHS), wahamiaji wanaweza kurushwa kimabavu katika nchi maskini ikiwa maafisa wa uhamiaji ama wana hakikisho “za kweli” kidiplomasia hawatakandamizwa au kuteswa ikiwa watarushwa huko au wamepatia wahamiaji notisi ya muda mfupi wa hadi saa sita kabla ya wakati ambao wanatoswa pahali kama hapo.