Kimataifa

Trump abadilisha Wizara ya Ulinzi kuwa Wizara ya Vita

Na MASHIRIKA September 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON DC, AMERIKA

RAIS Donald Trump aliweka saini, Ijumaa, kubadilisha jina la Wizara ya Ulinzi kuwa Wizara ya Vita, na kurejelea jina lililotumika hadi baada ya Vita vya Pili vya Dunia wakati maafisa walipoafikiana kusisitiza jukumu la Pentagoni katika kuzuia machafuko.

Hatua ya Trump inawakilisha juhudi zake za hivi karibuni kubadilisha jeshi la Amerika, ambazo zimejumuisha uamuzi wake wa kuongoza gwaride la jeshi Washington, DC, na kurejesha majina asilia ya ngome za jeshi zilizobadilishwa baada ya maandamano ya kutetea asili mbalimbali mnamo 2020.

Trump vilevile alikaidi kanuni za kawaida kuhusu kutuma vikosi vya ulinzi nchini, kwa kubuni maeneo ya kijeshi kwenye mpaka wa kusini na Mexico ya kuwezesha msako wa wahamiaji haramu na kuvituma vikosi katika miji kama vile Los Angeles na Washington.

Pentagon ilibadilisha upesi nembo kwenye makao makuu ya jeshi la Amerika yenye pembe tano mijini Arlington, na Virginia, na cheo cha Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth kilichopachikwa kwenye lango lake kuwa “Waziri wa Vita” na anwani ya naibu wake Steve Feinberg, kuwa ‘Naibu Waziri wa Vita’.

“Ni mabadiliko muhimu mno, kwa sababu ni mtazamo,” Trump alipoweka saini Amri ya Rais kwenye hafla iliyofanyika Oval Office.

“Inahusu kushinda.”

Hatua hiyo ingeagiza Hegseth kupendekeza hatua za kisheria na kiusimamizi zinazohitajika kufanya mabadiliko hayo ya majina kuwa ya kudumu.

Mabadiliko ya majina ya wizara ni nadra na yamekuwa yakihitaji kuidhinishwa na bunge.

Hata hivyo, Trump alisaili ikiwa kweli alihitaji kibali cha bunge, hata ingawa wanachama wenzake wa Republican wanashikilia idadi ya walio wengi bungeni kwa viti vichache tu katika Seneti na Bunge la Kitaifa.

Maseneta wawili wa Republican, Mike Lee (Utah) na Rick Scott (Florida), na mbunge wa Republican, Greg Steube (Florida), waliwasilisha sheria hiyo Ijumaa kufanya mabadiliko hayo.

Waziri Hegseth, aliyetambulishwa na Trump kama Waziri wa Vita, alishangilia mabadiliko hayo ambayo amepigia debe kwa muda mrefu.

“Tunaelekea mashambulizi, sio tu ulinzi. Ukali kikamilifu sio sheria fufutende,” alisema Hegseth.

Wizara ya Ulinzi Amerika iliitwa Wizara ya Vita hadi 1949, wakati bunge liliunganisha Jeshi la Ardhi, Jeshi la Majini na Jeshi la Anga wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Wanahistoria wanasema jina hilo liliteuliwa kwa kiasi fulani kuashiria katika enzi ya nuklia, Amerika itatilia maanani kuzuia mapigano kwa juhudi zote.

Itakuwa ghali kubadilisha majina tena na itahitaji kubadilisha saini, anwani za barua zinazotumiwa na maafisa sio tu Pentagon, bali vilevile vituo vya kijeshi kote ulimwenguni.

Juhudi za aliyekuwa rais Joe Biden kubadilisha ngome tisa za kijeshi zilizojengwa kwa heshima ya viongozi waliowezesha muungano wa majimbo zilikadiriwa kugharimu jeshi Sh5.05 bilioni.

Hegseth alibatilisha juhudi hizo mwaka huu.

Wakosoaji wamesema mpango wa kubadilisha majina ni ghali na unatatiza Pentagon.

Hegseth alisema kubadilisha jina “sio kuhusu maneno tu – inahusu kanuni za mashujaa vilevile.”

Mwaka huu, mwenyekiti wa Kamati ya Uangalizi, James Comer wa Republican ambaye ni moja kati ya wandani wakuu wa Trump, aliwasilisha mswada uliorahisisha rais kugeuza na kubadilisha majina ya mashirika.