Kimataifa

Trump aendelea kupondwa kwa kutuma wanajeshi kukabili maasi dhidi ya utawala wake

Na MASHIRIKA August 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIKU moja baada ya kutisha kutumia wanajeshi kuzima maasi dhidi ya utawala wake jijini Chicago, jimbo la Illinois Rais Donald Trump ametuma wanajeshi katika mji wa Baltimore, jimboni Maryland kutekeleza kibarua hicho hicho.

Hatua hiyo huenda ikaendeleza uhasama kati ya rais huyo na Gavana wa jimbo hilo Wes Moore, baada ya kiongozi huyo wa chama cha Democratic kumwalika kwa “matembezi ya usalama” jijini Baltimore.

“Ikiwa Wes Moore anahitaji usaidizi jinsi Gavin Newscum [Newsom] alihitaji Los Angeles, nitatuma wanajeshi kufagia haraka uhalifu nilivyofanya katika jiji la Washington DC,” Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii Jumapili.

Kauli hiyo ya hivi punde inayoashiria juhudi za Trump kutuma vikosi vya Jeshi la Kitaifa katika majimbo yanayoongozwa na magavana wa chama cha upinzani cha Democrat katika kile anachotaja kama vita dhidi ya uhalifu.

Hatua ya Trump kutumia wanajeshi kukabiliana na raia wanaoandamana kupinga uongozi wake, imepingwa vikali ya wafuasi wa Democrat.

Gavana mmoja alitaja hatua hiyo kama “matumizi mabaya ya mamlaka.”

Tayari Trump ametuma wanajeshi 2,000 jijini Washington DC, ngome ya chama cha Democrat.

Mnamo Jumapili, wanajeshi walianza kubeba silaha kuendesha operesheni jijini Washington, kulingana na makao makuu ya jeshi.

Awali, silaha zao zilihifadhiwa katika maghala yao, ambapo zingetumika tu endapo haja maalum ingetokea; na kama hatua ya mwisho.

Wanajeshi wengine 1, 700 wanatarajiwa kutumwa katika majimbo 19 ndani ya wiki chache zijazo, kulingana na vyombo vya habari nchini Amerika.

Gavana Moore wa jimbo la Maryland, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa mbinu hii ya rais kutumia wanajeshi kupambana na maasi ya ndani, alisema kauli ya Trump kwamba anapambana na uhalifu “hayana mashiko.”

“Ni kwa sababu hawajatembea katika barabara zetu. Hawajatangamana na watu wetu na ndio maana wanazungumza mabaya kutuhusu,” akaeleza.

Kauli ambayo Trump alitoa kupitia mtandao wa Truth Social Jumapili, ilionekana kujibu barua ya mwaliko kutoka kwa Moore ambayo Rais huyo aliitaka kama “mbaya na ya kuchokoza”.

“Kama Rais, ningemtaka kumaliza janga hilo la uhalifu kabla nifike huko kwa ‘matembezi’,” Trump akaandika.

Ikulu ya White House inasema kuwa mamia ya watu wemekamatwa tangu operesheni ya jeshi ilipoanza jijini Washington DC.

Akiongea katika Ikulu hiyo Ijumaa, Trump alisema wanajeshi hao walileta “usalama kamili” jijini Washington.

“Washington iligeuka kuwa jehanamu. Lakini sasa iko salama,” akaeleza.

Kulingana na takwimu za uhalifu zilizochapishwa na Kitengo cha Polisi wa Jiji la Washington DC (MPDC) visa vya uhalifu vilipungua baada ya kuongezeka mnamo 2023. Na mnamo 2024, visa hivyo vilishuka zaidi ndani ya miaka 30 iliyopita.

Katika mwaka huu wa 2025, kulingana na MPDC visa hivyo vinaendelea kupungua.