Trump afaulu kushawishi Zelensky kukubali Amerika ichimbe madini Ukraine

WASHINGTON, AMERIKA
UKRAINE na Amerika Jumatano zilitia saini mkataba ambao utawezesha serikali ya Rais Donald Trump kuchimba madini na kushiriki mchakato wa kujenga upya Ukraine.
Nchi hizo mbili zilitia saini mkataba huo jijini Washington baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo ambayo nusura yasambaratike kutokana na kukosekana kwa muafaka hapo awali.
Mkataba huo unaiweka Amerika na kibarua kikali cha kujenga upya Ukraine hatua hiyo pia ikitarajiwa kuimarisha juhudi za kupatikana kwa amani kwenye vita kati ya Ukraine na Urusi.
Maafisa wa serikali ya Ukraine wana wingu la matumaini kuwa Amerika sasa itawaunga mkono kwenye vita dhidi ya Urusi.
Waziri wa Fedha wa Amerika Scott Bessent na Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Yulia Svyrydenko walitia saini makubaliano hayo.
Katika mkataba huo, Amerika imeahidi kuhakikisha Ukraine inangáa na inakuwa taifa huru ambalo halijasambaratishwa na vita.
Svyrydenko aliandika kwenye ukurasa wake wa X kwamba Amerika itakuwa inatoa mchango wa kifedha na pia kupiga jeki Ukraine kijeshi.
Amerika imekuwa ikifaa Ukraine kwa hali na mali tangu 2022 wakati ambapo nchi hiyo iliingia kwenye vita na Urusi. Inakisiwa Amerika imetumia zaidi ya Sh9.3 trilioni kwa ajili ya Ukraine tangu vita hivyo vianze.
Kabla ya kutiwa saini kwa mkataba huo, Rais Trump Jumatano alisema nchi yake lazima ipate faida au tunu kutokana na jinsi ambavyo imeunga mkono Ukraine kivita ikitumia rasilimali zake.
Ukraine ina utajiri wa madini hasa chuma ambazo zinatumika kutengeneza vifaa vya kielektroniki, magari ya kielektroniki, silaha za kijeshi.
Kando na chuma za thamani pia ina gesi ya asili na madini ya urani (uranium).
Amerika imekuwa ikiunga mkono Urusi itwae eneo la Crimea, ambalo ilichukua kutoka Ukraine mnamo 2014 ili iongezee maeneo mengine manne.
Hata hivyo, Rais Zelenskiy amesema hawatakubali hilo kwa sababu inakiuka katiba ya Ukraine.