Trump ajiunga na TikTok aliyoipiga vita
NA MASHIRIKA
WASHINGTON, Amerika
RAIS wa zamani wa Amerika Donald Trump mnamo Juni 1, 2024, alijiunga na mtandao wa TikTok na kufuatiliwa na watu 3 milioni.
Itakumbukwa kwamba akiwa rais kati ya 2016 na 2019, Trump alijaribu kupiga marufuku matumizi ya mtandao huo wa kijamii kwa misingi ya usalama wa kitaifa.
“Ni kwa heshima yangu,” Trump akasema kwenye video aliyoituma katika mtandao huo akionenakana akipungia hadhira mkono katika hafla moja ya michezo katika mji wa Newark, ulioko jimbo la New Jersey, Amerika.
Ujumbe wake wa kwanza aliouweka katika mtandao huo pia ulitazamwa mara 33 milioni ndani ya saa 12 na sasa kupendwa (likes) mara 2.9 milioni.
Wakati huu, Trump anazongwa na kesi kadha mahakamani, ambazo zinadaiwa kuyumisha kampeni zake.
Mnamo Alhamisi wiki jana, alikuwa rais wa zamani wa kwanza katika historia ya Amerika kushtakiwa na kupatikana na hatia na mahakama.
Mnamo Alhamisi wiki jana Trump alipatikana na hatia kwa makosa 34 ya kuvuruga rekodi za kibiashara kwa lengo la kuficha ushahidi kwamba alimlipa mchezaji filamu mmoja za ngono ili asifichue uhusiano wake naye kimapenzi, miezi michache kabla ya uchaguzi wa urais wa Novemba 2016.
Rais Joe Biden, ambaye ni mpinzani mkuu wa Trump katika uchaguzi wa urais utakaofanyika Novemba 2024, alifungua akaunti yake ya TikTok mnamo Februari 2024.
Tayari akaunti hiyo inafuatiliwa na zaidi ya watu 340,000.
Lakini mnamo Aprili 2024, Biden alitia saini mswada wa kupiga marufuku TikTok baada ya Bunge la Congress na lile la Seneti kuupitisha.
Kupigwa marufuku kwa TikTok kulitokana na tishio la kiusalama kwa misingi kuwa unamilikiwa na kampuni ya ByteDance kutoka China.
Hatua hiyo ilipingwa vikali ndani na nje ya Amerika, huku watu wakisema hatua hiyo ni kinyume na kipengele cha Katiba kinachoruhusu ushindani wa haki.
Maelezo zaidi na Charles Wasonga