Kimataifa

Trump ashindwa katika rufaa ya kesi ya ubakaji aliyotozwa mabilioni

Na MASHIRIKA December 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA ya rufaa, Jumatatu iliidhinisha uamuzi kwamba Rais Mteule wa Amerika Donald Trump alipe dola  5 milioni (Sh650 milioni) ambazo E. Jean Carroll alishinda dhidi yake kwa unyanyasaji wa kijinsia na baadaye kumchafulia jina mwandishi huyo wa zamani wa gazeti.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya pili ya Rufaa Amerika huko Manhattan, kwa pamoja  lilikataa hoja ya Trump kwamba jaji wa mahakama hakufaa kuwaruhusu wachunguzi kusikiliza ushahidi kuhusu madai ya utovu wa nidhamu dhidi yake.

Mahakama ilisema kwamba ushahidi, ikiwa ni pamoja na Trump kujivunia uwezo wake wa ngono kwenye video ya “Access Hollywood” iliyojitokeza wakati wa kampeni za urais Amerika mwaka wa 2016, ilithibitisha “mtindo wa kurudiwa na wa kijinga”  unaokubaliana na  madai ya Carroll.

“Tukichukua rekodi kwa ujumla na kuzingatia nguvu ya kesi ya Bi Carroll, hatushawishiwi kwamba makosa yoyote yanayodaiwa au mchanganyiko wa makosa katika uamuzi wa mahakama ya wilaya uliathiri haki kubwa za Bw Trump,” mahakama ilisema katika uamuzi ambao haujatiwa saini.

Hukumu ya Mei 2023 ilitokana na tukio la 1996 katika chumba cha kubadilishia nguo cha duka la Bergdorf Goodman huko Manhattan, ambapo Carroll, ambaye sasa ana umri wa miaka 81, alisema Trump alimbaka, na chapisho katika mtandao wa kijamii wa Truth mnamo Oktoba 2022 ambapo Trump alikanusha madai ya Carroll kama mzaha.

Ingawa majaji katika mahakama ya shirikisho huko Manhattan hawakugundua kuwa Trump, 78, alibaka, walimtunuku mwandishi huyo wa zamani wa jarida la Elle dola 2.02 milioni (260 milioni) kwa unyanyasaji wa kijinsia na dola 2.98 (390 milioni) milioni kwa kuchafuliwa jina

Mahakama tofauti iliamuru Trump mnamo Januari amlipe Carroll dola 83.3 milioni (11 bilioni) milioni kwa kumkashifu na kumharibia sifa mnamo Juni 2019, alipokanusha madai yake ya ubakaji kwa mara ya kwanza.

Katika kukanusha kwake mara mbili, Trump alisema hamjui Carroll, hakuwa “aina yangu,” na kwamba alitunga madai ya ubakaji ili kukuza kumbukumbu yake.

Steven Cheung, msemaji wa Trump, alisema katika taarifa yake kwamba Waamarika “wanataka kukomeshwa mara moja kwa mfumo wetu wa haki kutumiwa kama silaha ya kisiasa na kutupiliwa mbali kwa kesi zote za nia mbaya, pamoja na ya mzaha ya  Carroll anayefadhiliwa na chama cha Democratic, ambayo itaendelea katika rufaa.”

Haikuwa wazi ikiwa rufaa yoyote itafika Mahakama ya Juu ya Amerika. Trump alimchagua Cheung mwezi uliopita kuwa mkurugenzi wake wa mawasiliano katika Ikulu ya White House.

Roberta Kaplan, wakili wa Carroll, alisema katika taarifa: “E. Jean Carroll na mimi tumefurahishwa na uamuzi wa leo.”

Kesi za Carroll zinaendelea licha ya Trump kushinda muhula wa pili wa miaka minne kama Rais wa Amerika.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA