Kimataifa

Trump asitisha msaada wa kijeshi Ukraine

Na REUTERS March 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON DC, AMERIKA

RAIS wa Amerika, Donald Trump amesimamisha msaada wa kijeshi Ukraine, siku chache tu baada ya makabiliano ya hadharani kati yake na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House.

Hii ni baada ya Trump mapema Jumatatu kukana uwezekano wa Amerika kusitisha msaada wa kijeshi wakati alipoulizwa na waandishi wa habari.

Hatua hiyo sasa inaiweka Ukraine pabaya kwani huenda sasa ikashindwa kabisa kukabiliana na uvamizi wa Urusi.

Afisa mmoja wa Ikulu ya White House Jumanne alisema Trump amekuwa wazi kuwa lengo lake ni amani na kwamba anahitaji washirika wake kujitolea katika lengo hilo pia.

Alisema serikali inasitisha kwa muda na kutathmini msaada wake kwa Ukraine ili kuhakikisha kuwa unachangia katika kupata suluhu ya kudumu.

“Rais Trump amekuwa wazi kuwa anaangazia amani. Tunahitaji washirika wetu kujitolea kwa lengo hilo pia. Tunasimama na kukagua misaada yetu ili kuhakikisha kuwa italeta suluhu,” afisa huyo alisema Jumatatu, akizungumza kwa sharti la kutotajwa.

Ikulu ya White House hata hivyo haikutoa maoni kuhusu hilo wala haikutaja kiasi cha misaada iliyoathiriwa au muda wa kusitishwa kwa misaada.

Kwa upande mwingine, ofisi ya Zelenskiy pia haikujibu mara moja ombi la Reuters la kutoa maoni na vile vile Ubalozi wa Ukraine huko Washington.

Hata hivyo, imeripotiwa kuwa kusitishwa huko kumeanza kutekelezwa mara moja.

White House ilisema agizo hilo litatekelezwa hadi Trump atakapoamua kuwa Ukraine imeonyesha kujitolea kwake kufanya mazungumzo ya amani na Urusi.

Utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joe Biden uliipatia Kyiv zaidi ya Sh8.5 trilioni katika msaada wa kijeshi na silaha tangu vita kuanza.

Ulikuwa imebakisha takriban Sh497 bilioni katika ufadhili ulioidhinishwa na bunge ya kupeleka silaha zaidi kwa Ukraine kutoka kwa hifadhi zilizopo za Amerika- kiasi ambacho hakikuwa kimeathiriwa na hatua ya kufungia misaada ya kigeni ambayo Trump aliweka wakati alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza.

Zelensky alisema Jumatatu kuwa anataka vita hivyo vimalizike haraka iwezekanavyo.

Mapema Jumatatu, Trump alimkosoa vikali Zelensky kwa kupendekeza kwamba vita hivyo huenda vikaendelea kwa muda.

Rais huyo wa Amerika alijibu kwenye mtandao wake wa Truth Social, akisema kuwa matamshi hayo yalikuwa mbaya zaidi na kwamba Amerika haingevumilia kwa muda mrefu zaidi!”

“Ni kile nilichokuwa nikisema, mtu huyu hataki kuwe na amani mradi tu anaungwa mkono na Amerika na viongozi wa Ulaya. Katika mkutano wetu, Zelensky alikiri kwamba hawawezi kushinda vita hivyo bila usaidizi wa Amerika,” alisema Trump.

Trump amedokeza kuwa Zelensky “hatadumu kwa muda” ikiwa rais huyo wa Ukraine hatakubali makubaliano ya kusitisha mapigano na Moscow.