Kimataifa

Trump atakataa kutengwa licha ya kutangamana na wanaougua corona

March 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

RAIS Donald Trump wa Marekani amekataa kujitenga licha ya kutangamana na watu ambao waliwakaribia wengine waliothibitishwa kuugua virusi vya corona.

Wabunge Doug Collins wa Georgia na Matt Gaetz wa Florida majuzi walitangaza watajitenga baada ya kufahamishwa walitangamana kwa karibu na mtu ambaye baadaye alipatikana kuambukizwa virusi hivyo.

Hayo yalitokea wakati wa kongamano kubwa la kisiasa mwezi uliopita.

Collins alimsalimia Trump Ijumaa, na Gaetz alisafiri naye kwenye gari rasmi la rais kabla ya kusafiri pamoja katika ndege ya Air Force One mnamo Jumatatu.

Ni wakati wa safari hiyo ya ndege ambapo Gaetz alifahamishwa na waandalizi wa kongamano alilohudhuria awali kwamba alikaribiana sana na mtu aliyeambukizwa.

“Aliposhuka ndege, alipimwa mara moja,” afisi yake ikasema.

Mkuu wa wafanyakazi katika Ikulu ya White House anayetarajiwa kuchukua usukani Mark Meadow pia alijitenga baada ya kuhudhuria kongamano hilo.

Seneta Ted Cruz wa Texas nchini Marekani pia amejitenga.

Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno mnamo Jumapili alitengwa baada ya kutangamana na mwanafunzi ambaye baadaye aligunduliwa ameambukizwa virusi hivyo.

Ikulu ya rais ilisema pia kuwa Trump hajapimwa virusi vya corona licha ya kutangamana na wabunge hao ambao wanashuku huenda waliambukizwa ugonjwa huo.

Katibu wa habari katika White House Stephanie Grisham, alisema Trump hajapimwa kwa sababu hajaonyesha dalili zozote za kuugua.

“Rais Trump ni buheri wa afya na daktari wake anaendelea kumchunguza kama kawaida,” akasema.

Alieleza kwamba mwongozo rasmi kuhusu matibabu ya virusi vya corona ni kwamba madaktari wanapaswa kumpima mtu ikiwa ameonyesha dalili za kuugua au kwa kuzingatia alivyotangamana na wagonjwa.

Mapema, Makamu wa Rais Mike Pence alisema hajui kama Trump alipimwa. Pence ndiye anayeongoza jopo la kukabiliana na virusi vya corona nchini humo.

Alisema pia yeye mwenyewe hajapimwa ugonjwa huo kwa vile hapajakuwa na pendekezo lolote kwamba apimwe.

Kufikia jana watu zaidi ya 116,000 kote duniani walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo huku zaidi ya 4,000 wakiaga dunia.

China inaendelea kuongoza kwa visa vingi vingi vya maambukizi na vifo ikifuatwa na Italia.