Trump atisha kuwahepa wanahabari wanaomuuliza 'maswali ya kipuuzi'
MASHIRIKA na PETER MBURU
RAIS wa Marekani Donald Trump ametishia kuwa atakuwa akihepa kutoka vikao na waandishi wa habari ikiwa hawatamheshimu na kumuuliza maswali bila kumvamia.
Kupitia ujumbe wa barua ambayo ilimrejeshea mwanahabari wa Shirika la CNN Jim Acosta idhini ya kufanya kazi tena katika ikulu ya White House, Rais Trump alilalamika kuwa wanahabari wamekuwa wakikosa mpangilio na maadili wanapomhoji.
Bw Acosta alikuwa amepokonywa idhini ya kuingia ikulu wiki mbili zilizopita baada ya majibizano na Rais Trump wakati wa kikao cha mahojiano na wanahabari.
Shirika la CNN ambalo Bw Acosta anafanya kazi nalo limekuwa likitofautiana na namna ya uongozi wa Rais Trump, jambo ambalo lilichangia tofauti baina yao.
Hata hivyo, Ijumaa wiki iliyopita Jaji mmoja Marekani aliamrisha ikulu kumrejeshea mwanahabari huyo idhini, akisema kumpokonya ilikuwa sawa na vita dhidi ya uhuru wa wanahabari.
Lakini ikimrejeshea Bw Acosta idhini hiyo, ikulu ilitangaza kuja na sheria mpya ambazo “zitaongoza vikao vya mahojiano siku za usoni.”
Sheria hizo zinahusisha kila mwanahabari kuuliza swali moja pekee, ambalo linajisimamia. Barua hiyo iliendelea kusema kuwa ikiwa mwanahabari atahitaji ufafanuzi, ni Raisa ma afisa wa Ikulu atakayeamua ikiwa utatolewa.
Katika kikao hicho cha Novemba 8, Rais Trump alimtaja Bw Acosta kuwa “Jeuri”, kisha siku iliyofuata akakatazwa kuingia ikulu.
Shirika la CNN pamoja na mengine ya habari yaliishtaki ikulu na Ijumaa korti ikaamua kuwa hakukuwa na sababu zilizofaa kumpokonya mwanahabari huyo idhini yake kuingia ikulu.
Hata hivyo, mashirika ya habari nchini humo yamekosoa sheria mpya ambazo ikulu inawataka kufuata, yakidai japo maadili yamesisitizwa, Rais mwenyewe hana maadili mema ya uhusiano na watu kwani mbeleni amekuwa akiwapuuza wanahabari kuwa wanauliza ‘maswali ya kipuuzi’.