Kimataifa

Trump atishia ‘kuua’ uchumi wa Urusi ikikataa kukomesha vita na Ukraine

Na MASHIRIKA January 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON, AMERIKA

RAIS wa Amerika Donald J Trump Jumatano alitishia Urusi, akisema kuwa ataongezea nchi hiyo vikwazo zaidi iwapo haitaridhia kuafikia mkataba wa kumaliza vita kati yake na Ukraine.

Kiongozi huyo alisema kuwa vikwazo hivyo pia vitalenga mataifa ambayo yanaunga Urusi katika vita hivyo, matamshi yaliyoonekana kulenga Korea Kaskazini.

Mnamo Jumanne, Rais Vladimir Putin alimwonya vikali Rais wa Urusi Vladimir Putin akisema hafai kukataa kufika kwenye meza ya majadiliano ambayo itasaidia kumaliza vita hivyo ambavyo vimedumu kwa miaka mitatu.

“Iwapo hatutafikia mkataba hivi karibuni, sitakuwa na budi ila kuweka vikwazo vingi na ushuru wa juu kwa kila kitu ambacho Urusui inauza kwa Amerika. Adhabu hii pia itawaendea washirika wake kwenye vita hivyo,” akasema Rais Trump.

Utawala wa Aliyekuwa Rais Joe Biden uliweka ushuru mwingi kwa Urusi kwenye sekta za utengenezaji bidhaa, kawi, teknolojia, ulinzi, benki. Adhabu hizo zilianza tangu Februari 2022 wakati ambapo Urusi ilivamia Ukraine.

Vita kati ya Ukraine na Urusi vimechangia mauaji ya maelfu ya watu na kulemazi miji mbalimbali ambayo sasa imesalia vigae.

Naibu Balozi wa Urusi katika Shirika la Umoja wa Kimataifa (UN) Dmitry Polyanskiy alisema italazimu Urusi kusubiri ili kuona mbinu ambayo Rais Trump anafikiria zaidi itasaidia kumaliza vita hivyo.

“Hoja si kumaliza tu vita hivyo bali ni kuangazia uchokozi wa Ukraine na msingi wao wa kudai baadhi ya maeneo ya Urusi mpakani,” akasema Polyanskiy.

Kuelekea ushindi wake wa Nov 5, Rais Trump wakati wa kampeni alikariri kuwa akiingia afisini, siku yake ya kwanza itakuwa kuziamrisha Ukraine na Urusi kusitisha vita na kukumbatia maelewano.

Ingawa hivyo, wandani wake wamekiri kuwa mkataba wa kumaliza vita hivyo huenda ukachukua miezi kadhaa kuafikiwa kutokana na msimamo mgumu kati ya nchi hizo mbili.

Mapema mwezi huu, Amerika iliweka ushuru mkubwa zaidi kwa sekta za mafuta na gesi pamoja na meli 183, hatua ambayo ilipunguza zaidi mapato ya Urusi katika sekta hiyo ya kawi.

Rais Putin amekiri kuwa uchumi wa nchi hiyo umekuwa ukifanya vibaya tangu waingie vita na Ukraine lakini akasisitiza kuwa hawatashurutisha kuingia kwenye mkataba ambao utasababisha waachilie mipaka yao.

Kando na Urusi, Rais Trump pia analenga kutumia vikwazo na ushuru kutishia Mexico, Canada na China ili kuwashinikiza wazime uhamiaji haramu.