Kimataifa

Trump awashangaza walimwengu kulia kuibiwa kura kabla ya hesabu

November 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., Amerika

RAIS Donald Trump alishangaza ulimwengu Jumatano alipojitokeza kutangaza kwamba ameshinda kura nyingi za uchaguzi wa urais, hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa.

Zaidi ya hayo, Trump alidai wizi wa kura ulikuwa unaendelezwa ili kumpendelea mpinzani wake wa karibu, Joe Biden, wa chama cha Republican.

Aliiomba Mahakama ya Juu kuingilia kati ili kusimamisha shughuli ya kuhesabu kura.

Hadi tukienda mitamboni, wawili hao walikuwa wanaendelea kukabana koo kwa idadi ya kura ambazo zilikuwa zinaendelea kutangazwa katika majimbo mbalimbali.

Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi walisema huenda hesabu ya mwisho ikachelewa mwaka huu kwa sababu kura nyingi zilitumwa kwa shirika la posta na itachukua muda mrefu kuzihesabu zote.

Katika hali iliyoonekana kama ukiukaji wa taratibu za uchaguzi nchini humo, Trump alidai uwepo wa “udanganyifu mkubwa” huku akifanya mkutano mdogo katika Ikulu ya White House, alikokuwa akifuatilia matokeo hayo.

“Tumeibuka washindi kwenye uchaguzi huu,” akasema Trump, alipowahutubia wafuasi wake wachache waliokongamana, japo wakizingatia masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

“Huu ni udanganyifu wa wazi kwa raia wa Amerika,” akaeleza.

Kiongozi huyo alisema ataenda katika Mahakama ya Juu kwani “anataka taratibu zote za upigaji hesabu kusimamishwa.”

Hata hivyo, shughuli za upigaji kura tayari zilikuwa zimekamilika wakati ambapo alianza kuhutubu.

Trump alikuwa akieleza uwezekano wa wizi wa kura, hasa baada ya karibu raia 100 milioni wa taifa hilo kupiga kura zao kwa njia ya posta ili kuepuka kuambukizwa virusi vya corona.

Washirika wa Biden walipuuzilia mbali tishio la Trump, wakishikilia mawakili wao walikuwa tayari kumkabili kwenye mahakama.

“Taarifa ya Rais kuhusu tishio la kujaribu kusimamisha upigaji kura haifai na ni ukiukaji mkubwa wa sheria,” akasema meneja mkuu wa kampeni za Biden, Jen O’ Malley Dillon.

“Hatujawahi kusikia Rais wa Amerika akitishia kuwanyima raia haki ya kufanya maamuzi yao huru kwenye uchaguzi mkuu,” akaeleza.

Kauli hiyo ilijiri muda mfupi baada ya Trump kutoa hotuba isiyo ya kawaida katika Ikulu, akidai ushindi.

Hii ni licha ya wagombea wote wakuu kutofikisha kiwango kinachohitajika kikatiba ili mwaniaji kutangazwa mshindi.

“Tunataka shughuli ya kuhesabu kura kusimamishwa mara moja,” akasema Trump.

Kauli yake ilionekana kurejelea kura ambazo zilikuwa zimepigwa kwa njia ya posta.

Matokeo ya uchaguzi katika majimbo kadhaa muhimu bado hayakuwa yametangazwa mapema jana. Majimbo hayo ni Georgia, Michigan, Pennsylvania na Wisconsin.

Kwa muda mrefu, Biden amekuwa akionya kwamba lengo la Trump lilikuwa ni kupuuzilia mbali mfumo wa upigaji kura kwa kutumia posta ambao umetumika pakubwa kwenye uchaguzi huu.