Trump kukausha Kenya akiashiria kuondoa usaidizi wa kijeshi wa miaka mingi
RAIS wa Amerika Donald Trump ameashiria mabadiliko ya sera yaliyofaidi Kenya kupitia ufadhili wa kijeshi akiwaambia maafisa wakuu wa jeshi la nchi hiyo kuwa “si jukumu la jeshi la Amerika kulinda mataifa ya nje kama Kenya na Somalia.”
Katika hotuba yake kwa maafisa zaidi ya 800 wa ngazi ya juu wa kijeshi mnamo Jumanne, Trump alisema kuwa baada ya miongo kadhaa ya kampeni za kijeshi za kimataifa, sasa ni wakati wa jeshi kuangazia ulinzi wa nchi yao dhidi ya “adui aliye ndani” ambao hatambuliki kwa urahisi.
“Katika miongo ya hivi majuzi, wanasiasa waliamini kuwa jukumu letu ni kuwa polisi wa nchi za mbali kama Kenya na Somalia, huku Amerika ikiathirika na uvamizi kutoka ndani,” alisema Trump akiwa katika kambi ya jeshi la Marine Corps Quantico, Virginia.
Hali hii inaweza kuashiria mabadiliko katika sera za Washington, hasa ikizingatiwa kuwa makubaliano ya biashara ya Amerika na nchi kadhaa za Afrika chini ya mkataba wa AGOA yamekwisha bila tangazo lolote kutoka kwa utawala wa Trump.
Trump pia ameagiza jeshi kuwekwa katika miji mikubwa ya Amerika kama Los Angeles, Washington DC, Memphis, na Portland, huku akionyesha nia ya kupeleka wanajeshi katika miji kama San Francisco, Chicago, na New York, akifananisha hali hiyo na vita.
Kenya imekuwa mshirika wa karibu wa Amerika katika masuala ya ulinzi kwa miongo mingi, na mwaka jana tu ilitambuliwa na utawala wa Rais Joe Biden kama mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO.
Kenya pia ina kituo cha kijeshi cha Amerika huko Manda Bay, Lamu, ambacho kinatumika katika operesheni za kupambana na ugaidi katika Afrika Mashariki.
Mnamo Septemba 2023, Waziri wa Ulinzi wa Amerika Lloyd J. Austin III na Waziri wa Ulinzi wa Kenya wakati huo Aden Bare Duale walitia saini makubaliano ya miaka mitano ya ushirikiano wa kijeshi ya mamilioni ya pesa, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika teknolojia ya ulinzi, uvamizi wa kigaidi, mafunzo pamoja na usalama wa baharini.