Kimataifa

Trump kwa Zelensky: Kubali Crimea itwaliwe na Urusi amani ije Ukraine

Na REUTERS August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WASHINGTON, Amerika

RAIS wa Amerika Donald Trump ameiambia Ukraine kwamba sharti ikubali kuachilia eneo la Crimea endapo ingetaka kutia mkabata wa amani na Urusi.

Sharti lingine ni kwamba Ukraine ikomeshe ari yake ya kuwa mwanachama wa mataifa wanachama wa kundi la NATO.

Kwenye taarifa katika mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump alieleza kuwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky “anaweza kukomesha vita na Urusi mara moja akitaka au anaweza kuendelea kupigana.”

Rais huyo wa Amerika alisema hayo baada ya kukutana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, ambapo ilisemekana hawakukubaliana kuhusu kutiwa saini kwa mkataba wa amani.

Hata hivyo, Trump alisema mkutano huo ulikuwa ‘wenye manufaa makubwa zaidi’.

Kwa upande wake Rais Zelensky alishikilia, kupitia taarifa katika mtandao wa kijamii, kwamba “Sharti Urusi ikomeshe vita hivi, ilivyovianzisha.”

Zelensky aliratibiwa kukutana na Trump katika Ikulu ya White House Jumatatu, Agosti 18, 2025, akiandamana na viongozi kadhaa wa mataifa ya Uropa pamoja na Katibu Mkuu wa NATO Mark Ruttle.

Kabla ya kukutana na Putin Ijumaa wiki jana, Trump alikuwa ametisha kumchukulia “hatua kali” ikiwa hatashirikiana kuhusu suala hilo la mkataba wa amani.

Hata hivyo, baada ya mkutano huo alisisitiza kuwa haja yake kuu sasa sio kusitishwa kwa mapigano haraka, bali makubaliano ya amani ya kudumu.

Trump hajakuwa na uhusiano mzuri na Rais Zelensky, kwani mnamo Februari mwaka huu alimkosoa kiongozi huyo wa Ukrane hadharani alipomtembelea katika Ikulu ya White House.

Ukraine imekuwa ikishikilia kuwa ingetaka kukomesha vita hivyo vilivyodumu kwa miaka mitatu na nusu, kwa njia ya kudumu.

Mnamo Machi mwaka huu, nchi hiyo ilitia saini makubaliano ya kukomeshwa kwa vita, yaliyosimamiwa na Amerika, lakini Urusi ikakataa kutia saini yake.

Trump amewahi kudai kuwa Rais Barack Obama ndiye aliyechangia Ukraine kupoteza himaya yake ya Crimea huku akishikilia kuwa “Amerika haitakubali Ukraine kujiunga na NATO ikiwa itahitajika kusaidia katika kukomeshwa kwa vita Ukraine.”

Urusi ilitwaa Crimea, eneo lililoko kusini kwa Ukraine, mnamo 2014.

Hata hivyo, hatua hiyo haijatambuliwa rasmi kimataifa na Ukraine imekuwa ikisisitiza kuwa inalenga kurejesha himaya hiyo.

Baada ya hapo, Urusi ilitwaa maeneo ya mashariki mwa Ukraine ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia mnamo 2022, miezi michache kabla ya kufanya uvamizi kamili katika taifa hilo jirani yake.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA