Trump ni mhalifu, asema Ayatollah Khamenei akiapa ‘kumwadhibu’
KIONGOZI mkuu Ayatollah Ali Khamenei mnamo Jumamosi alimlaumu Rais wa Amerika, Donald Trump kwa majuma kadhaa ya maandamano yaliyosababisha zaidi ya vifo 3,000 kwa mujibu wa makundi ya kutetea haki za binadamu.
“Tunamchukulia rais wa Amerika kuwa mhalifu kwa wahasiriwa, uharibifu na kuchafulia jina alikosababishia taifa la Iran,” alisema Khamenei, kulingana na vyombo vya habari nchini humo.
Maandamano yaliyozuka Desemba 28 kuhusu hali ngumu kiuchumi yalilipuka na kuwa maandamano ya kuitisha mwisho wa utawala wa kidini katika Jamhuri ya Kiislamu.
Trump ametishia mara kwa mara kuingilia kati, ikiwemo kutishia “hatua kali zaidi” ikiwa Iran itawaua waandamanaji.
Lakini Ijumaa, katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii, aliwashukuru viongozi jijini Tehran, akisema wamefuta hukumu za kuwanyonga raia kwa pamoja. Iran ilisema “hakuna mpango wa kuwanyonga watu”.
Katika matamshi yaliyoonekana kumjibu Trump, Khamenei alisema: “Hatutaburura taifa kuingia vitani, lakini hatutaruhusu wahalifu wa humu nchini na kimataifa kwenda bila kuadhibiwa,” vyombo vya habari kutoka nchini humo vilisema.
Katika mahojiano na gazeti la Politico mnamo Jumamosi, Trump alisema “wakati umewadia kutafuta uongozi mpya Iran” na kuitisha mwisho wa utawala wa miaka 37 wa Khamenei.
Trumo, katika mahojiano tofauti na Reuters Jumatano wiki iliyopita, alisema kiongozi wa upinzani nchini, Reza Pahlavi “anaonekana mzuri sana” lakini akaashiria wasiwasi kuhusu iwapo Pahlavi ataweza kuvutia uungwaji mkono nchini ili kuchukua usukani hatimaye.