Kimataifa

Tshisekedi akataa mkutano wa Ruto kujadili kutekwa kwa Goma

Na MASHIRIKA January 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Félix Tshisekedi, Jumatano alikataa kushiriki katika mazungumzo yaliyoitishwa na Rais William Ruto wa Kenya ya kujadili kutekwa kwa jiji la Goma na waasi wa M23, Shirika la Habari la Serikali nchini humo liliripoti.

Rais Ruto alikuwa amemwalika Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kwenye mkutano wa mtandaoni jana, huku maiti zikiwa zimetapakaa katika barabara za jiji la Goma kufuatia mapigano makali.

Rwanda inalaumiwa kwa kuunga mkono kundi la waasi wa M23, ambalo limeteka sehemu kubwa ya mji huo, ukiwemo uwanja wa ndege.

Mnamo Jumanne Kagame aliashiria kuwa anaunga mkono kusitishwa kwa mapigano kufuatia mazungumzo yake na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika, Marco Rubio.Umoja wa Mataifa unasema kuna ushahidi mkubwa kwamba Rwanda inaunga mkono M23 lakini nchi hiyo inakanusha madai hayo.

Jiji la Goma lilikuwa tulivu kiasi Jumatano, kukiwa na ripoti za milio ya risasi hapa na pale katika baadhi ya maeneo.

Wakazi ambao walikuwa wamejificha katika maeneo salama walijitokeza kununua chakula ambacho kinazidi kuwa haba kufuatia mapigano.

Shirika rasmi la habari la DR Congo lilisema kuwa Tshisekedi hatahudhuria mkutano ulioitishwa na Ruto kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Haikutoa sababu za Rais huyo kukataa kushiriki mkutano huo.