Tshisekedi na Kagame wakubali kukutana kujadili amani mashariki mwa DRC
NA PATRICK ILUNGA
KINSHASA, DRC
RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, wamekubaliana kukutana na kujadili jinsi ambavyo mapigano mashariki mwa dRC yanavyoweza kusitishwa.
Hata hivyo, kila mmoja alimshutumu mwenzake kwa kuhujumu juhudi za kuzima mapigano hayo ambayo yamedumu kwa miaka 30 iliyopita.
Katika siku za hivi karibuni mapigano hali ya utovu wa usalama katika eneo hilo la mashariki wa DRC imechochewa zaidi na uhasama kati ya marais hao wawili.
Rais wa Angola Joao Lourenco, balozi wa Umoja wa Afrika (AU) wa eneo la Maziwa Makuu na wapatanishi wengine, majuzi walijaribu kuhimiza pande mbili hasimu kukumbatia mazungumzo.
Mnamo Alhamisi, ujumbe wa maafisa wa serikali za DRC na Rwanda ulikutana jijini Luanda, Angola kuandaa mkutano kati ya marais Tshisekedi na Kagame.
Lakini mnamo Jumanne katika mahojiano na shirika la habari la Jeune Afrique, Rais Kagame alimshutumu mwenzake kwa kusababisha “hali ya kutoelewana katika eneo hili” kati ya viongozi hao na kati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Kusini (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Rais Kagame alikosoa jinsi mwenzake wa DRC anavyoshughulikia mpango wa kuleta amani, kwa kuyaacha nje baadhi ya makundi ya waasi kama M23 na badala yake kuwakabili wapiganaji wake kwa kutumia nguvu, akishirikiana na wanajeshi wa SADC.
Kimsingi, AU, SADC na EAC zimekuwa zikishirikiana kufufua mazungumzo kati ya Tshisekedi na Kagame na ikizekana, kati ya waasi.
Mashirika ya kikanda na yale ya kimataifa yanahimiza kufufuliwa upya kwa michakato ya amani inayoongozwa na Angola na Kenya.
Mchakato unaoongozwa na Angola unalenga kufanikisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya DRC na Rwanda ilhali ule wa Kenya unalenga kufanikisha mazungumzo kati ya serikali ya DRC na makundi ya wapiganaji mashariki mwa nchi hiyo.
Michakato hiyo miwili inaonekana kusambaratika au kusitishwa.
Lakini hali ya kutoaminiana bado upo.
Rais Kagame anawashutumu wanajeshi DRC na wale wa jumuia ya SADC kwa kushirikiana na kundi la wapiganaji la FDLR wanaoendesha mashambulio mashariki mwa DRC. Wapiganaji hao wanajumuisha wale walioshiriki katika mauaji ya halaiki ya 1994 nchini Rwanda.
Mwenyekiti wa jumuiya ya EAC na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Jumatatu alikamilisha ziara yake jijini Kinshasa, DRC ambapo alikutana na Rais Tshisekedi.
Ziara hiyo ni sehemu ya kile kinachotajwa kama “ziara ya amani” iliyoanzia Rwanda na Burundi mnamo Februari mwaka huu.
Taarifa ya pamoja ya EAC iliyotolewa kutoka jijini Kinshasa ilieleza kuwa Rais Kiir na Tshisekedi “walitoa wito kusuluhishwe mzozo kuhusu sekritariati ambao umeathiri utendakazi wa jumuiya hiyo.”
“Marais hao wawili walitaka michakato ya amani ya Kenya na Angola ifufuliwe upya iliyoazishwa na EAC na AU, mtawalia,” taarifa hiyo ikaongeza.
Huku michakato ya amani ikitarajiwa kurejelewa mapigano mapya yalizuka katika mji wa Sake, katika na mji Goma katika mkoa wa Kivu Kaskazini.