Kimataifa

Tumeua kiongozi wa 7 wa Hezbollah, Israel yajigamba

Na REUTERS September 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JERUSALEM, ISRAEL

ISRAEL imetangaza kuwa imemuua kiongozi mwingine wa ngazi ya juu wa kundi la Hezbollah katika shambulio la angani huku kundi hilo la wapiganaji likizongwa na msururu wa maafa.

Jeshi la Israel lilisema Nabil Kaouk, naibu kiongozi wa Baraza Kuu la Hezbollah aliuawa Jumamosi jioni.

Uongozi wa kundi hilo la wapiganaji ulithibitisha kifo cha afisa huyo ambaye ni kiongozi wa saba wa Hezbollah kuuawa katika mashambulio yaliyotekelezwa na Israel ndani ya majuma mawili yaliyopita.

Miongoni mwa waliouawa ni wanachama waanzilishi waliokwepa kifo au kifungo gerezani kwa miongo kadhaa.

Jeshi la Israel lilisema kuwa lilitekeleza shambulio jingine jijini Beirut mnamo Jumapili jioni, japo halikutoa maelezo zaidi.

Awali, Hezbollah ilithibitisha kuwa Ali Karaki, kamanda mwingine mkuu, alikufa katika shambulio la Ijumaa lililoua kiongozi wake mkuu Hassan Nasrallah.

“Karaki aliuawa katika shambulio lililolenga handaki fulani jijini Beirut ambako Nasrallah na viongozi wengine wakuu wa Hezbollah walikuwa wanakutana,” jeshi la Israel likasema kwenye taarifa.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa angalau wapiganaji 20 wa Hezbollah waliuawa katika shambulio hilo, wakiwemo wasaidizi wawili wa Nasrallah, mmoja wao akiwa msimamizi wa walinzi wake.

Mabaki ya majumba yaliyoshambuliwa bado yalikuwa yakiteketea zaidi ya siku mbili baadaye.

Mnamo Jumapili, wanahabari waliona moshi ukifuka katika vifusi hivyo huku watu wakikongamana katika eneo la tukio.

Wengine walifika kubaini hali ya nyumba zao huku wengine wakifika kufanya maombi au kujionea kiwango cha uharibifu.

Kufikia Jumapili jumla ya watu 1,030 walikuwa wameuawa katika sehemu mbalimbali nchini Lebanon, kufuatia msururu wa mashambulio ya Israel, ndani ya muda wa wiki mbili.

Miongoni mwa waliouwa ni wanawake 156 na watoto 87, kulingana na Wizara ya Afya nchini humo.

Vilevile, maelfu ya watu wametoroka makwao nchini Lebanon kutokana na mashambulio yaliyotekelezwa siku chache zilizopita.

Serikali inakadiria kuwa takriban watu 250, 000 wanaishi katika makazi ya muda huku wengine wengi wakiishi na marafiki au jamaa zao au wanakaa kando ya barabara.

Hii ni kulingana na Waziri wa Mazingira Nasser Yassin.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi (UNICEF) lilisema zaidi ya watu 70, 000 wamevuka mpaka na kuingia Syria kujiepusha na madhara ya mashambulio ya Israel.

Idadi hiyo inajumuisha pia raia wa Syria ambao walikuwa wamehamia Lebanon lakini sasa wameamua kurejea nchini mwao.

Wakati huo huo, Hezbollah imeendelea kurusha roketi na makombora kaskazini mwa Israel lakini mengi yamedunguliwa au kuanguka maeneo yasiyoishi watu.

Hamna raia wa Israel aliyeuawa tangu kuanza kwa msururu wa hivi punde wa mashambulio yaliyoanza Septemba 20 na kulenga viongozi wakuu wa Hezbollah.

Kaouk alikuwa mwanachana mkuu wa Hezbollah tangu 1980.

Amewahi kuhudumu kama kamanda wa kijeshi wa kundi hilo kusini mwa Lebanon wakati wa vita kati ya nchi hiyo na Israel mnamo 2006.