Uchaguzi mswaki kwa Ouattara upinzani ukizimwa Cote d’Ivoire
ABDIJAN, COTE D’IVOIRE
RAIS Alassane Ouattara, 83, anatarajiwa kuwahi ushindi baada ya mpinzani wake mkuu mwingine kukatazwa kushiriki kura kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.
Mahakama ya Kikatiba ilimzuia Mfanyabiashara Tidjane Thiam na rais wa zamani Laurent Ghagbo kuwania kura hiyo.
Aliyekuwa mkewe Gbagbo, Simone naye ameidhinishwa kuwania uchaguzi huo.
Ouattara sasa anaonekana yupo pazuri kushinda baada ya kutangaza mnamo Julai kuwa anasaka muhula wa nne katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa Cocoa.
Thiam, alikuwa mwaniaji wa chama kikubwa cha upinzani cha PDCI na alionekana kama mwaniaji ambaye angemtoa kijasho rais wa sasa.
Aliondolewa kwenye kinyang’anyiro kwa kuwa wakati ambapo alikuwa akijisajili alikuwa pia na uraia wa Ufaransa.
Katiba ya Cote d’Ivoire inazuia mtu ambaye ana uraia wa mataifa mawili kugombea urais wa taifa hilo.
Wawaniaji watano sasa wameidhinishwa kuwania kati ya 60 ambao waliwasilisha stakabadhi zao kwa Tume ya Uchaguzi ya Cote d’Ivoire japo wanaonekana kama mswaki kwa Ouattara.
Kampeni rasmi zinatarajiwa kuanza mnamo Oktoba 10.
Pingamizi
Thiam na viongozi wengine wa upinzani wamekuwa wakipinga hatua ya Ouattara kuwania muhula wa nne.
Hata hivyo, rais huyo amekuwa akisema kuwa katiba mpya iliyorasimishwa mnamo 2016 inaamrisha kuwa mihula aliyokuwa amedumu hapo awali iondolewe na muda wa uongozi wake ukaanza kuhesabiwa upya.
Gbagbo alikataa kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 na ghasia zikazuka Cote d’Ivoire na kuchangia mauaji ya zaidi ya watu 3,000.
Alikamatwa na mkewe Simone japo rais huyo wa zamani alishtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) lakini hakupatikana na hatia.
Simone alihukumiwa na Mahakama ya Cote d’Ivoire kutokana na vita hivyo vya kijamii mnamo 2011 lakini Ouattara akampa msamaha wa rais mnamo 2018.
Anaonekana kama mpinzani rahisi kwa rais huyo ikilinganishwa na Thiam na Gbagbo.