Kimataifa

Uchumi wa Tanzania kukua kuliko wa Kenya, Uganda

February 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

UCHUMI wa Tanzania umetabiriwa kukua kuliko chumi za Kenya na Uganda mwaka huu 2024.

Kulingana na ripoti iliyotolewa Jumatano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 6.1, kiwango ambacho ni cha juu, ikilinganishwa na mataifa mengine katika ukanda wa Afrika Mashariki, isipokuwa Rwanda.

Kwenye ripoti ‘Tathmini ya Ustawi wa Kiuchumi’ (MEO), uchumi wa Rwanda ndio utakua kwa kiwango cha juu zaidi mwaka huu Afrika Mashariki, kwa asilimia 7.2

Tanzania pia imeorodheshwa nambari tisa miongoni mwa mataifa 11 bora ambayo chumi zake zitakua kwa kiwango cha juu zaidi mwaka huu barani Afrika.

Mataifa hayo ni: Niger (asilimia 11.2), Senegal (asilimia 8.2), Libya (asilimia 7.9), Rwanda (asilimia 7.2), Cote d’ Ivoire (asilimia 6.8), Ethiopia (asilimia 6.7), Benin (asilimia 6.4 na Djibouti (asilimia 6.2).

Mataifa yanayofuata ni Togo na Uganda, yaliyotabiriwa kukua kwa kiwango cha asilimia sita kila moja.

Kulingana na mkuu wa benki hiyo, Dkt Akinwumi Adesina, kiwango cha ukuaji wa wastani barani Afrika kitakuwa asilimia 3.8.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya kiuchumi, utathmini huo ni wa kutamausha nchini, hasa wakati ambapo serikali imekuwa ikielezea kuhusu mikakati iliyoweka katika kuboresha uchumi wa nchi.

Pia, hayo yanajiri wakati Wakenya wengi walikuwa washaanza kuonyesha matumaini ya gharama ya maisha kupungua, baada ya thamani ya shilingi ya Kenya kuanza kuimarika dhidi ya sarafu za kigeni, kama vile dola ya Amerika.

Kwa sasa, dola ya Amerika inauzwa kwa Sh144,  baada ya kushuka kutoka Sh160 siku 10 zilizopita.

Wadadisi wanasema utathmini huo unafaa kuwaamsha Wakenya, kwamba kuna hatari kubwa Kenya kupoteza nafasi yake kama taifa lenye uchumi mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Kwa muda mrefu, Kenya imekuwa ikiorodheshwa kama taifa lenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki. Hata hivyo, hali inaonekana kubadilika, kwani mataifa ambayo yamekuwa yakidharauliwa, kama vile Tanzania, yameanza kuamka kiuchumi,” asema mdadisi wa masuala ya kiuchumi, Bw Tony Watima.