Uganda yaagiza intaneti izimwe katika kipindi cha uchaguzi mkuu
SERIKALI ya Uganda imeagiza huduma za intaneti ndani na nje ya nchi zizimwe katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Januari 15, 2026.
Tangazo la Tume ya Mawasiliano nchini humo ‘Uganda Communication Commission’ la Januari 13, 2026 linasema kwamba hatua hii imeafikiwa baada ya “mapendekezo makubwa kutoka kwa Kamati ya Usalama” kuhusu uwezekano wa matumizi ya mitandao kuzua taharuki wakati wa kura hiyo.
Marufuku hiyo inaanza kutekelezwa saa 12 jioni, Januari 13, 2026.
Rais Yoweri Museveni anatafuta muhula wa saba huku akiadhimisha miaka 40 mamlakani, baada ya kutwaa hatamu za uongozi 1986.
SOMA PIA: Museveni pazuri kushinda muhula wa saba licha ya kampeni kali za Bobi Wine
Anakabiliwa na upinzani kutoka kwa wawaniaji saba ingawa mwaniaji wa chama cha National Unity Platform, msanii wa zamani Bobi Wine, 43, ameonekana kuchangamsha zaidi wapigakura vijana.
Hata hivyo, wachanganuzi wanashikilia kwamba uchaguzi huo utakuwa mswaki kwa mkongwe Museveni kwa jinsi ambavyo amedhibiti taasisi nyingi muhimu katika taifa hilo.
Huduma za intaneti zilizozimwa zinajumuisha mawimbi ya ndani ya nchi, uuzaji na ununuzi wa kadi mpya za simu pamoja na intaneti ya kutoka nje kwenda ndani almaarufu ‘roaming services’.
“Hatua hii ni muhimu katika kudhibiti usambazaji wa habari potovu, ulaghai wa kura pamoja na kuzuia uchochezi ambao unaweza kuathiri mshikamano wa taifa,” ikasema taarifa hiyo.
Katika uchaguzi wa urais wa 2021, Bobi Wine alipata asimilia 35 ya kura na vijana wanamshabikia wakimuona kama suluhu ya matatizo ya ukosefu wa ajira na kukithiri kwa ufisadi.
Rais Museveni ameifanyia mageuzi Katiba ya Uganda mara mbili kuondoa hitaji la umri na lile la kumtaka rais kuongoza kwa mihula mahsusi.
SOMA PIA: Bobi Wine: Nimeteswa ya kutosha ila sitakufa moyo, lazima Museveni aondoke