Kimataifa

Uganda yawazia kuanza kuwanyonga mashoga

October 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

HOFU imetanda Uganda baada ya Waziri wa Maadili nchini humo kutangaza kuwa nchi hiyo inapanga kurejesha sheria iliyozua utata kuhusu ushoga ambayo iliharamishwa na mahakama ya kikatiba 2014.

Simon Lokodo aliwaambia wanahabari kwamba mswada huo utaanzishwa upya na watakaopatikana na hatia watakuwa wakihukumiwa kunyongwa.

“Sheria zetu za sasa kuhusu uhalifu ni dhaifu. Zinaeleza tu kuwa kitendo hicho ni cha kihalifu. Tunataka ieleweke wazi kuwa yeyote anayehusika na kutangaza au kusajili watu kuwa washoga anatenda uhalifu. Wale wanaotekeleza kitendo hicho watahukumiwa kunyongwa,” alisema Lokodo.

Aliongeza kuwa ushoga si tabia asili ya raia wa Uganda na watu wamekuwa wakisajiliwa kwa wingi katika shule. Pia wapo wanaoeneza habari za uongo kuwa kuna wanaozaliwa wakiwa mashoga.

Mnamo Februari 2014, Rais Yoweri Museveni alitia sahihi sheria iliyojulikana kama “Ua Mashoga” ili kutoa adhabu kali kwa wanaohusika na mapenzi ya jinsia moja.

Mahakama ya kikatiba ya Uganda ilibatilisha sheria hiyo baadaye mwaka huo ikisema kwamba wabunge waliipitisha bila idadi inayohitajika bungeni.

Bw Lokodo anasema yuko tayari kwa kampeni ya kupinga hatua yake. Alisema mswada huo mpya utawasilishwa bungeni wiki chache zijazo na una ‘baraka’ za Rais Museveni na wabunge.

Waziri huyo aliambia runinga ya NTV Uganda kwamba ana imani mswada huo utaungwa mkono na thuluthi mbili ya wabunge.

Miezi mitano iliyopita, mataifa kadhaa ya Ulaya na Amerika yalisimamisha misaada nchini Uganda kufuatia kampeni dhidi ya ushoga. Bw Lokodo alisema Uganda imejiandaa kwa chochote kwa sababu ya kampeni yake dhidi ya ushoga.

“Hatutaki kutishwa. Ingawa tunajua hii itawakasirisha wanaotusaidia katika bajeti na utawala, hatuwezi kuinamia wanaotaka kutusukumia desturi za kigeni.”

Katika sheria za Uganda ambazo zilibuniwa wakati wa utawala wa ukoloni, adhabu ya kushiriki ushoga ni kufungwa jela maisha na wanaharakati wanasema mswada huu mpya unaweza kufanya mashoga kuanza kushambuliwa.

Pepe Julian Onziema kutoka shirika la Sexual Minorities Uganda, ambalo linashirikiana na muungano wa kutetea haki za mashoga na wasagaji (LGBT) alisema wanachama wake wanaishi kwa hofu.

“Sheria hiyo ilipopitishwa wakati uliopita, ilizua chuki na uhasama dhidi ya watu walioshukiwa kuwa mashoga,” alisema Bw Onziema.

“Maelfu ya wanachama wa LGBT wamelazimika kutoroka nchi hii na kuishi kama wakimbizi katika nchi nyingine na wengi watawafuata sheria ikibuniwa,”alisema.

Bw Onziema alisema mwanamume mmoja shoga na mwanamke huntha waliuawa mwaka 2018 nchini Uganda kwenye mashambulizi dhidi ya mashoga.

Wiki jana, mwanamume shoga aliuawa kwa kupigwa kwa rungu.