Uhaba wa bidhaa wanukia Uganda agizo la kuzima intaneti likikwamisha mizigo Kenya
WAHUDUMU wa mizigo katika Bandari ya Mombasa wamesitisha usafirishaji wa mizigo inayoelekea Uganda na nchi nyingine zisizo na bandari, saa chache baada ya taifa hilo kuzima huduma ya intaneti kabla ya Uchaguzi Mkuu wa leo.
Mawakala wa kuthibitisha na kuondoa mizigo bandarini pamoja na wasafirishaji walisema hatua ya mamlaka za Uganda kuzima intaneti kitaifa ilikatiza mawasiliano kati yao na madereva, na kuvuruga taratibu za kuunda nyaraka na uidhinishaji wa mizigo.
Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Kimataifa cha Usafirishaji Mizigo na Uhifadhi wa Maghala nchini (KIFWA), Bw Fredrick Aloo, alisema sekta hiyo hutegemea sana intaneti na mizigo haiwezi kusonga bila mawasiliano.
“Intaneti inapozimwa, uratibu unakuwa mgumu zaidi, ufuatiliaji na uwasilishaji wa nyaraka unachelewa, na safari huchelewa,” alisema Bw Aloo.
Mbali na mawasiliano, Bw Aloo alisema mizigo ya kusafirishwa kwenda nchi jirani hutegemea vifaa vya ufuatiliaji vya GPRS vinavyotuma taarifa kupitia data ya simu na intaneti.
“Bila intaneti kuna hatari ya msongamano mkubwa katika vituo vya mipakani,” akasema.
Mnamo Jumanne, serikali ya Uganda iliagiza kampuni za mitandao ya simu kufunga huduma ya intaneti ya umma kuanzia saa kumi na mbili jioni huku shirika la kufuatilia matumizi ya intaneti, NetBlocks, baadaye likithibitisha kuwepo kwa “usumbufu wa kitaifa wa huduma ya intaneti”.
Bw Roy Mwanthi, msafirishaji wa mizigo kutoka Mombasa, alisema kwa sasa anaelekeza juhudi zake katika kusafirisha mizigo ya ndani ya nchi hadi baada ya uchaguzi.
“Mizigo ambayo tayari imeidhinishwa kwa safari ya nje ya nchi itasafirishwa hadi mipaka ya Busia na Malaba, lakini ili kuhakikisha usalama na kuepuka hasara, tutaelekeza nguvu zetu kwenye mizigo ya ndani,” alisema.
Uchaguzi huo wa urais unaonekana kama marudio ya kinyang’anyiro cha mwaka wa 2021, ambapo Rais Yoweri Museveni, 81, ambaye amekuwa madarakani kwa miongo minne, anakabiliwa tena na mpinzani wake mkuu, mwanamuziki Bobi Wine, 43, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi. Kuna wagombeaji wengine sita.
Mamlaka ya mawasiliano ilitetea uamuzi wake kwa msingi wa usalama wa umma ili kuzuia “upotoshaji wa taarifa mtandaoni, habari za uongo na udanganyifu wa uchaguzi, pamoja na kuzuia uchochezi wa vurugu”.
Mapema mwezi huu, mamlaka hiyo ilipuuza habari zilizokuwa zikienea kuhusu uwezekano wa kuzimwa intaneti wakati wa uchaguzi ikidai kuwa ni uvumi, na kusema jukumu lake ni kuhakikisha mawasiliano yanapatikana bila kukatizwa kote nchini.
Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2021, ambao ulighubikwa na maandamano makubwa yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa, huduma ya intaneti ilikatizwa kwa angalau wiki moja.
Hali sawa na hii ilishuhudiwa mwaka uliopita wakati vurugu zilipotokea baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania, ambapo pia wasafirishaji mizigo kati ya Kenya na nchi hiyo jirani walitatizika katika mipaka kama vile Lunga Lunga na Taveta.