Kimataifa

Ujerumani yaonya Trump dhidi ya kuvamia Greenland

Na REUTERS January 11th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

BERLIN, UJERUMANI

KANUNI za sheria ya kimataifa zinatumika kwa wote, ikiwemo Amerika, Waziri wa Fedha na Naibu Chansela, Lars Klingbeil, alisema Jumapili, Januari 11, 2026 akirejelea vitisho vya Rais Donald Trump kuhusu kuteka taifa la Greenland.

“Uamuzi kuhusu hatima ya Greenland upo mikononi mwa Denmark na Denmark pekee. Hadhi na uadilifu kimaeneo ni sharti iheshimiwe,” alisema Klingbeil kabla ya kusafiri kuelekea Washington kwa mkutano wa mawaziri wa fedha kutoka mataifa makuu duniani (G7) yenye mifumo iliyoendelea kiuchumi.

Hatua ya jeshi la Amerika kupokonya Denmark kisiwa hicho chenye utajiri itatikisa mkataba baina ya Amerika Kaskazini na Uropa (NATO) na kuzidisha utengano kati ya Trump na viongozi wa Uropa.

“Tunaongeza usalama katika ukanda huo pamoja kama wandani wa NATO, sio katika upinzani dhidi yetu,” alisema Klingbeil.

Mkutano wa G7 utakaofanyika Jumatatu utaangazia upatikanaji wa madini muhimu huku nchi za Magharibi zikinuia kupunguza kutegemea China kwa kuzingatia hatua za Beijing kuanzisha vidhibiti vikali kuhusu uuzaji wa madini adimu katika mataifa ya kigeni.

Klingbeil alisema Ujerumani inataka kupanua ushirikiano kimataifa eneo hili ili kuimarisha usalama wa bidhaa, kupunguza utegemezi na kuhakikisha mazingira ya mfumo wa uchumi yanayoweza kutegemewa.

“Ndiposa ni muhimu tushauriane na washiriki wetu kimataifa na kila inapowezekana –tuchukue hatua pamoja,” alisema.

China inatamalaki mfumo wa kusambaza madini adimu, huku ikisafisha kati ya asilimia 47 na 87 ya shaba, lithiamu, kobalti, graphite na madini adimu, kulingana na Shirika la Kimataifa kuhusu Nishati.