Kimataifa

Ulaya kusuka mpango wa amani Ukraine baada ya Trump kumfukuza Zelensky White House

Na MASHIRIKA March 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema viongozi wa Ulaya wamekubali kuandaa mpango wa kuleta amani Ukraine, ambao utawasilishwa kwa Amerika.

Hatua hiyo itawezesha Amerika kutoa usaidizi wa kiusalama ambao Ukraine inasema ni muhimu sana katika kuzuia vita vya Urusi.

Katika kongamano jijini London, Uingereza — siku mbili baada ya Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kutofautiana wazi wazi na Rais Donald Trump wa Amerika kabla kukatiza ziara yake nchini Amerika — viongozi wa Ulaya walijitokeza kuunga mkono rais wa Ukraine na wakaahidi kufanya mengi zaidi kusaidia taifa lake.

Aidha, viongozi wa Ulaya walikiri kuwa sharti wawekeze fedha nyingi zaidi katika sekta zao za ulinzi ili kuonyesha Trump kwamba bara hilo linaweza kujilinda.

Starmer, ambaye alimlaki Zelensky kwa kumpiga pambaja alipowasili Uingereza mnamo Jumamosi, alieleza kwamba taifa lake, Ukraine, Ufaransa na mataifa mengine yataunda mpango wa amani ambao watampelekea Trump.

“Huu sio wakati wa mazungumzo zaidi, ni wakati wa vitendo. Wakati wa kuungana kuendeleza mpango utakaohakikisha kuwepo kwa amani ya kudumu,” Starmer akasema.

Hata hivyo, viongozi hao wa Ulaya hawakutoa maelezo ya kina kuhusu mpango wao.

Kabla kongamano hilo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliambia gazeti la Le Figaro kuwa mpango huo utahusu kipindi cha mwaka mmoja cha kusitisha vita angani na majini bali sio ardhini.

Wanajeshi wa mataifa ya Ulaya watatumwa Ukraine ikiwa mkataba kamili wa amani utaafikiwa, Macron alieleza.

Haijulikana ikiwa mataifa mengine ya Ulaya yalikubaliana na vipengele hivyo.

Baada ya kongamano Rais Zelensky alikuwa mwepesi kusema kuwa ameondoka London na “uungwaji mkono wa wazi kutoka Ulaya” akikariri kujitolea kwake kushirikiana na mataifa yote kumaliza vita baina ya taifa lake Ukraine na Urusi ambavyo vimedumu miaka mitatu sasa.

“Kutakuwa na mazungumzo ya kidiplomasia kwa lengo la kupatikana kwa amani,” akasema Zelensky kwenye hotuba yake kupitia video.

“Na kwa nia ya umoja wetu sote: Ukraine, mataifa yote ya Ulaya na bila shaka Amerika,” akaongeza.