UN: Takriban 800 wameuawa Gaza wakisubiri misaada
GENEVA, USWIZI
SHIRIKA la Kutetea Haki la Umoja wa Kitaifa (UN) jana lilisema kuwa zaidi ya watu 798 wameuawa kwenye Ukanda wa Gaza katika maeneo ambako vituo vya kutoa vyakula vya msaada vinapatikana.
Vituo hivyo vinaendeshwa na wakfu wa kutoa misaada ya kibinadamu Gaza Humanitarian Foundation ambao unasimamiwa na Amerika pamoja na Israel.
Maafa pia yameshuhudiwa karibu na vituo vingine vya kutoa misaada vinavyoendeshwa na mashirika mbalimbali ikiwemo UN yenyewe.
GHF imekuwa ikitumia vyombo vya usalama vya Amerika pamoja na kampuni zinazopeleka msaada Gaza.
Hata hivyo, shirika hilo halijakuwa likifuata taratibu ambazo ziliwekwa na UN kufikisha msaada Gaza.
Israel imepinga taratibu hizo ikisema zimetumika kuwafaa wanamgambo wa Hamas ambao wanapigana vita nao.
UN imekashifu Amerika na Israel kwa kukiuka mwongozo wa haki za kibinadamu na kuchangia maafa mengi katika Ukanda wa Gaza.
“Kufikia Julai 7 watu 798 walikuwa wameuawa Ukanda wa Gaza; 615 walikuwa karibu na vituo vya GHF na 183 walikuwa wakisubiri kupewa vyakula,” ilisema taarifa ya Ravina Shamdasani anayesimamia shughuli za usambazaji misaada ya UN katika ukanda huo.
GHF ilianza kusambaza misaada kwa wahanga wa kivita Gaza mwisho wa mwezi Mei japo imekanusha kuwa mauaji yametokea katika vituo vyake.