UN yayataka mataifa yaliyostawi yasaidie Afrika Mashariki kupambana na nzige
Na DIANA MUTHEU
UMOJA wa Mataifa (UN) umeiomba nchi zilizoendelea kusaidia Afrika Mashariki kupambana na nzige.
Wadudu hawa wameharibu vyakula katika nchi za Kenya, Somalia na Ethiopia; huu ukitajwa kama uvamizi mwingine wa nzige baada ya miaka 25 katika eneo la upembe wa Afrika.
Akizungumza katika kikao siku ya Jumapili, Katibu Mkuu wa UN, António Guterres alisema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yameathiri sana nchi katika Bara la Afrika.
“Joto jingi limeshuhudiwa kote ulimwenguni kwa miaka 10 iliyopita. Bara la Afrika halichangii sana katika mabadiliko ya hali ya hewa lakini nchi zake huteseka sana janga linapotokea ambalo limesababishwa na mabadiliko hayo. Nchi hizo zinahitaji msaada ili ziweze kudhibiti changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa,”alisema Bw Guterres.