Kimataifa

Upinzani na wanaharakati waandamana kulalamikia uamuzi wa Ouattara kugombea urais

August 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

ABIDJAN, Ivory Coast

VIONGOZI wa upinzani na mashirika ya kijamii nchini Ivory Coast waliandamana katika barabara za jiji kuu Abidjan kulalamikia uamuzi wa Rais Alassane Ouattara wa kugombea urais kwa kipindi cha tatu kwenye uchaguzi utakaofanyika Oktoba.

Barabara kuu jiji hilo zilifungwa na waandamanaji wakachoma magurudumu ya magari wakikabiliana na polisi waliowarushia gesi ya kutoa machozi.

Maandamano hayo yalianzia kati kati ya nchi hiyo mapema wiki hii na yameenea nchini ingawa polisi na wanajeshi wamefaulu kutawanya waandamanaji.

Upinzani umekasirishwa na tangazo Ouattara wiki jana kwamba atagombea urais kwa kipindi cha tatu.

Chama tawala kilimteua kuwa mgombeaji wake wa urais kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Amadou Coulibaly aliyekuwa amepatiwa tiketi ya kugombea kiti hicho. Coulibaly alifariki baada ya kupata mshtuko wa moyo.

Mnamo Machi, Ouattara aliahidi hatagombea urais tena. Hata hivyo, wiki jana alisema kifo cha Coulibaly kiliacha pengo ambalo alilazimika kujaza.

Anadai kwamba kwa kuwa katiba ilibadilishwa 2016, vipindi alivyokuwa amehudumu havihesabiwi katika Katiba ya sasa.

Viongozi wa upinzani wanamtaka ajiondoe na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ajiuzulu.

Msemaji wa muungano wa Coalition for Reconciliation, Democracy and Peace, Aka Ahizi, alisema uamuzi wa Ouattara unakiuka Katiba ambayo anafaa kutetea.