• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Upinzani waungana dhidi ya Magufuli kura zikikaribia

Upinzani waungana dhidi ya Magufuli kura zikikaribia

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, Tanzania

VYAMA vikuu viwili vya upinzani nchini Tanzania vimeamua kubuni muungano ‘legevu’ na kuteua kwa pamoja mgombea atakayeshiriki chaguzi za Oktoba 28 katika kila eneo.

Wapigakura katika maeneo ya bara Tanzania na visiwani Zanzibar wataelekea kwenye shughuli ya upigaji kura katika muda wa wiki mbili zijazo kuwachagua marais wao, wabunge na madiwani kote nchini humo.

Vyama hivyo vimechukua hatua hiyo katika jitihada za kubandua mamlakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimekuwa uongozini kwa miongo kadhaa.

Mwenyekiti wa chama cha upinzani Chadema, Freeman Mbowe, alisema majuzi kuwa chama chake kitamwondoa mgombea wake wa urais Zanzibar na kumuunga mkono Sharif Hamad, wa chama cha ACT-Wazalendo, dhidi ya mgombea wa CCM, Hussein Mwinyi.

Tangazo hilo lilijiri wiki mbili tu baada ya mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha ACT-Wazalendo, Hamad, kusema chama chake kitamuunga mkono mgombea wa Chadema, Tundu Lissu katika kinyang’anyiro hicho barani kumkabili Rais John Magufuli.

Tangu hapo, viongozi kadhaa kutoka vyama vyote viwili kama vile Zitto Kabwe wa ACT-Wazalendo na Salum Mwalimu, wa Chadema wamekuwa wakipigia debe wagombea wa ubunge na udiwani katika mikutano mbalimbali ya kampeni.

Kando na kutofautiana kuhusu jinsi ya kugawana nyadhifa, kuna suala lingine ambalo limezuia vyama hivyo kuweka rasmi ushirikiano wao.

Kulingana na sheria Tanzania, vyama vinavyotaka kubuni muungano rasmi vinahitajika kutia sahihi mkataba angalau siku 90 kabla ya uchaguzi kufanyika, na mkataba huo kuidhinishwa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa nchini humo.

Japo muungano usio rasmi huwa hauonekani kama unaokiuka sheria, Msajili wa Vyama vya Kisiasa mwezi uliopita aliwaonya maafisa wa vyama dhidi ya kuidhinisha wagombea wa vyama vya wenzao.

Miezi kadhaa iliyopita, vyama kadhaa vidogo vidogo vya upinzani vilijitokeza kuwaunga mkono wagombea wa chama tawala cha CCM.

Wakati huo, miungano hiyo haikukosolewa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa, lakini ilani za kurejelea hatua hiyo zimetolewa kufuatia onyo kwa ACT-Wazalendo na Chadema.

Wanasiasa wa Upinzani wamedai mara kwa mara kuhusu kuhangaishwa na serikali katika kampeni zao, ikiwemo kufutiliwa mbali kwa mamia ya wagombea ubunge dhidi ya kuwania katika chaguzi zijazo.

Mwanahabari wa Zanzibari na mchanganuzi wa kisiasa Salma Said aliashiria kuungana kwa ACT-Wazalendo na Chadema huku kukiwa na visa vingi vya kufutilia mbali wagombea, hali inayotarajiwa kudhoofisha ngome za vyama hivyo viwili vikuu vya upinzani.

  • Tags

You can share this post!

Afueni Sukuma Bin Ongaro akijengewa nyumba

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa zinazofanya isimu kuwa...