Urusi yafanya mazoezi ya zana za nyuklia huku mkutano wa Trump na Putin ukitibuka
MKUTANO uliokuwa ukitarajiwa kufanyika kati ya marais Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin jijini Budapest umesitishwa kwa muda.
Hii ni baada ya Putin kushindwa kukubaliana na suala la kusitishwa kwa mapigano kati ya Urusi na Ukraine.
Kando na hayo, Trump alisema kuwa hataki ‘kupoteza’ muda wake katika mazungumzo ambayo hayatazaa matunda.
Taarifa iliyotolewa Jumanne, Oktoba 21, 2025, na afisa mmoja wa serikali ya Washington ambaye hakutaka kutajwa, ilisema kuwa mkutano uliokuwa ukitarajiwa kufanyika kati ya marais hao wawili nchini Hungary umesitishwa kwa muda baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika, Marco Rubio kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov na kushindwa kuafikiana kuhusu suala nyeti la kusitisha mapigano katika nchi yake na Ukraine.
Trump amethibitisha taarifa hiyo akisema hatahudhuria mkutano wa kupoteza muda akiongeza pia kwamba kwa sasa wanasubiri kuona kitakachofuata akisisitiza kuwa pande zote zinaendelea kupata hasara kubwa kwa kuwapoteza wanajeshi wao na ndio maana amani inahitajika.
Lakini upande wa Moscow umesema maandalizi ya mkutano huo kati ya Trump na Putin yanaendelea na kwamba wanahitajika kukubaliana kuhusu mambo kadhaa muhimu.
Viongozi wa Ulaya wakiwemo wale kutoka Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Ulaya wakishirikiana na Ukraine walitoa taarifa ya pamoja siku ya Jumanne wakitaja kuunga mkono wito wa Trump wa kusitisha mapigano kati ya Urusi na Ukraine.
Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa viongozi hao wa Ulaya akiwemo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky watakutana Ijumaa wiki hii mjini London katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kujadili namna ya kuendelea kuiunga mkono Kyiv.
Haya yanajiri huku watu sita Ukraine wakiangamia kufuatia mashambulio ya makombora ya Urusi na ndege zisizo na rubani.
Watu wengine 21 pia walijeruhiwa, katika usiku mwingine wa mashambulio ambayo Zelensky alisema yalithibitisha kuwa Moscow haikuwa chini ya shinikizo la kutosha kwa kuendelea kwa vita.
Huku hayo yakijiri jeshi la Ukraine limasema kuwa limeshambulia kiwanda cha kemikali cha Urusi katika eneo la mpakani la Bryansk usiku wa Jumanne kwa kutumia makombora ya Storm Shadow yaliyotolewa Uingereza.
Shambulio hilo “lilipenya mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi”, maafisa wa jeshi la Ukraine walisema.
Kiwanda cha Bryansk “kinazalisha baruti, vilipuzi na vifaa vinavyotumika kutengeza roketi na makombora yanayotumiwa na adui kushambulia eneo la Ukraine.”