Kimataifa

Ushoga: Biden atupa nje Uganda katika mkataba wa kibiashara

January 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na VINCENT OWINO

AMERIKA imezima Uganda kufaidi kutokana na mpango wa kuruhusu mataifa ya Afrika kuuza bidhaa zao Amerika bila kulipia ushuru, kwa kupitisha sheria ya kupiga mafuruku ushoga.

Mataifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gabon na Niger pia yamewekewa marufuku kama hiyo japo kwa sababu za ukiukaji haki tofauti na zile za mashoga.

Kutokana na marufuku hiyo iliyotangazwa na Rais Joe Biden Desemba 29, 2023 baadhi ya bidhaa za Uganda hazitauzwa Amerika chini ya mkataba wa kibiashara uliotokana na Sheria ya Kuhusu Ustawi wa Afrika (AGOA).

Biden alisema, katika agizo lake, kwamba mataifa hayo manne ya Afrika hayajatimiza “mahitaji” ya kuyaruhusu kuendelea kufaidi kutokana na mkataba huo wa kibiashara, na hivyo kutimiza tishio lake la kuyapiga marufuku.

“Kwa hivyo, nimeamua kuondoa Jamhuri ya Afrika ya Katiba, Gabon, Niger na Uganda kutoka orodha ya mataifa ya Afrika ya kufaidi kutokana na manufaa ya sehemu ya 506A ya Sheria ya Biashara ya Agoa, kuanzia Januari 1, 2024,” ikasema taarifa iliyotolewa na Rais huyo wa Amerika.

Katika barua aliyomwandikia Spika wa Bunge la Congress mnamo Oktoba 2023, akielezea nia yake ya kuondoa nchi hizo nne kutoka orodha ya wafaidi wa Agoa Bw Biden alisema Uganda “imekiuka haki za kibinadamu zinazotambuliwa kimataifa.”

Hayo yalijiri baada ya Rais Yoweri Museveni kutia saini sheria inayopiga marufuku shughuli za ushoga baada ya kupitishwa na wabunge wa Uganda.

Sheria hiyo pia ilianzisha adhabu kali, ikiwemo kifungo cha maisha au kunyongwa, kwa mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja nchini humo.

Kufurushwa kwa Uganda kutoka mkataba huo wa Agoa kunatarajiwa kuchangia kupotea kwa nafasi nyingi za ajira, ukosefu wa fedha za kigeni na kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani, wataalamu wameonya.

Tangu kuanzishwa kwa sheria ya Agoa mnamo mwaka wa 2000 kuruhusu nchi za Afrika kuuza baadhi ya bidhaa zao nchini Amerika bila kulipia ushuru, Uganda imefaidi pakubwa kutokana na mpango huo.

Katika kipindi cha miezi 12 hadi Juni 2023, Uganda imeunza nchini Amerika bidhaa za thamani ya dola 8.2 (Sh1.27 bilioni) chini ya mkataba wa Agoa.

Hii ni sawa na asilimia 11.5 ya thamani ya bidhaa zote ambazo Uganda iliuzwa Amerika ndani ya kipindi hicho ambayo ni dola (Sh10,958 bilioni).

Hii ni kulingana na takwimu kutoka kwa Wizara ya Biashara nchini Amerika.

Zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa ambazo Amerika huu chini ya mkataba wa Agoa zilitoka sekta ya kilimo, ambayo huajiri asimilia 72 ya idadi jumla ya wafanyakazi Uganda.

Hii ina maana kuwa kufurushwa kwa Uganda kutoka Agoa kutachangia watu wengi kupoteza ajira.

Hata hivyo, kiwango cha kibiashara kati ya Uganda na Amerika ni kidogo ikilinganishwa na mataifa jirani zake kama vile Kenya na Tanzania.

Muda wa matumizi wa mkataba wa Agoa unatarajiwa kukamilika Desemba 2025. Hata hivyo, viongozi wa Amerika na maafisa wa wizara ya biashara wamelezea nia ya kuuongeza.

Uganda inaweza kurejeshwa katika mpango huo ikiwa itaonyesha nia ya kutimiza masharti yaliyowekwa; kwamba ibatilishe sheria inayopiga marufuku shughuli za ushoga.