Kimataifa

Utawala wa Donald Trump wajiandaa kwa awamu ya pili ya urais

November 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

IKULU ya White House inaendelea kuwapiga msasa watu ambao huenda wakahudumu katika muhula wa pili wa Donald Trump ambaye amekataa kushindwa uchaguzini.

Rais Trump amekuwa akitilia shaka matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo Novemba 3, yaliyoonyesha alishindwa na Joe Biden, aliyewania urais kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Duru zilieleza kwamba Afisi ya Masuala ya Wafanyakazi katika ikulu inaendelea kuwapiga msasa watu wanaotarajiwa kuhudumu kwenye nyadhifa mbalimbali serikalini.

Ikulu ilikuwa imepanga kujaza nafasi hizo kufikia mapema mwaka ujao. Afisi hiyo inaongozwa na John McEntee, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Trump.

Haya yote yanafanyika licha ya vyombo vya habari katika sehemu mbalimbali duniani kumtaja Biden kuwa mshindi halisi wa uchaguzi huo Jumamosi.

Ripoti zilieleza mwelekeo huo haunekani kuwashangaza wasaidizi wa maafisa wakuu wa serikali hiyo, kwani wanalazimishwa kuendesha majukumu yao kwa imani kwamba Rais Trump atahudumu kwa muhula mwingine wa miaka minne.

Jumanne, gazeti la ‘The Washington Post’ liliripoti kuwa “Afisi ya Kusimamia Bajeti katika White House iliziagiza idara kadhaa za serikali kuandaa makadirio ya bajeti ya utawala huo mwaka ujao.”

Wakati huo huo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni Mike Pompeo amesema wanaendeleza mchakato wa kuanzisha awamu ya pili ya uongozi wa Trump.

Hapo kesho, Pompeo ataelekea nchini Ufaransa kwa ziara maalum ya kikazi. Baadaye, atazuru mataifa ya Uturuki, Georgia, Israeli, Saudi Arabia, Milki ya Kiarabu (UAE) na Qatar. Nchi hizo ni washirika wa karibu wa Amerika.

Ziara hiyo itaonekana kama isiyofaa, kwani tayari Rais Trump amekataa kukubali kwamba alishindwa kwenye uchaguzi huo huku serikali yake ikidinda kuanza kuweka taratibu za kuwezesha kiongozi mpya kuchukua uongozi.

Biden alisema Jumanne kwamba misimamo ya Trump kukataa kukubali kushindwa ni aibu ambayo itamharibia sifa.

Alipoulizwa kuhusu ujumbe ambao angepitisha kwa Trump kama wangekutana, Biden alisema: “Bw Rais, ninatazamia kuzungumza nawe.”

Hata hivyo, alisema misimamo ya Trump haitaathiri mipango ya Democrat kujiandaa kuingia mamlakani.

“Serikali itabadilika ifikapo Januari 20, na kuanzia sasa hadi wakati huo, matumaini na matarajio yangu ni kuwa Waamerika wanajua na wanaelewa kwamba kutakuwa na serikali mpya,” akasema.