Kimataifa

Vatican yafichua kilichosababisha kifo cha Papa Francis

Na BENSON MATHEKA April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Makao Mkuu ya Kanisa Katoliki ulimwenguni,Vatican, imethibitisha rasmi kuwa Papa Francis, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Jorge Mario Bergoglio,  alifariki kutokana na kiharusi  kilichomfanya apoteze fahamu na hatimaye mshituko wa moyo usioweza kurekebishwa.

Cheti rasmi cha kifo kilitolewa na Dkt Andrea Arcangeli, Mkurugenzi wa Idara ya Afya na Usafi wa Vatican, ambaye pia alieleza kuwa Papa alikuwa na historia ya kiafya iliyojumuisha: Kushindwa kupumua  kutokana na nimonia ya pande zote mbili, pumu, shinikizo la damu la juu na kisukari.

Kifo chake kilithibitishwa kwa kutumia mfumo wa kielektroniki njia ya kisasa ya kuthibitisha kifo kwa kuchunguza shughuli za moyo.

Papa Francis alionekana mara ya mwisho  hadharani wakati wa Jumapili ya Pasaka Aprili  20 2025, ambapo alitoa baraka ya “Urbi et Orbi” katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, siku moja tu kabla ya kufariki dunia.

Kifo chake kimezua maombolezo makubwa duniani kote, huku viongozi wa dunia, viongozi wa kidini, na raia wakikumbuka urithi wake wa huruma, unyenyekevu, na kujitolea kwa haki ya kijamii.

Mkutano wa makadinali  kumchagua papa mpya unatarajiwa kuitishwa ndani ya siku 15–20.