Venezuela yasema iko tayari kukabili Amerika kivita
NA AFP
RAIS wa Venezuela Nicolas Maduro, ameyataka majeshi kuwa tayari wakati wowote ili kukabiliana na majeshi ya Marekani, huku utata kuhusu uongozi ukiendelea kushuhudiwa nchini humo.
Kiongozi wa Upinzani, Juan Guaido na Rais Maduro, wanaendelea kuonyeshana ubabe wa kisiasa, jaribio la mapinduzi majuma machache yaliyopita, likiwa kilele cha uhasama kati ya wawili hao.
“Nawaomba muwe tayari kulinda na kutetea nchi yenu kwa hali na mali. Tumieni silaha zenu kuyakabili majeshi ya Marekani ambayo ishara zote zinaonyesha yatavamia nchi yetu,” akasema Rais Maduro kwenye hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja kwenye runinga zote nchini Venezuela. Rais alikuwa ameandamana na Waziri wa Ulinzi Vladimir Padrino na wajeshi 5,000 waliojihami vikali.
Bw Guaido ambaye anaungwa mkono na zaidi ya mataifa 50 barani Uropa, amekuwa mwiba kwa serikali ya Rais Maduro tangu uchaguzi wa mwaka jana, anaodai alinyang’anywa ushindi na serikali ya sasa.
Akimjibu Rais Maduro, Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Marekani, Mike Pompeo naye aliwataka raia wa Venezuela kuendelea kuandaa maandamano makubwa dhidi ya utawala wa sasa.
“Wakati wa mabadiliko ni sasa. Unaweza kushikilia jeshi lako, vyombo vya usalama na makamanda wa majeshi lakini siku ya kuporomoka kwa utawala wako inakaribia
“Marekani inasimama na raia wa Venezuela na tunawaomba waendeleze juhudi za kuondoa serikali ya Rais Maduro mamlakani,” akasema Bw Pompeo.
Rais Maduro ameendelea kutotikisika kutokana na uungwaji mkono kutoka kwa wanajeshi hata baada ya jaribio hilo la mapinduzi lililosababisha vifo vya watu wanne na wengine wengi kujeruhiwa.
“Niliwaambia majenerali kwamba nategemea sana uaminifu wao. Hata hivyo, makinikeni na mkae ange ili wasaliti wachache wasituangushe na kuharibu jina letu,” akaongeza Rais Maduro kwenye hotuba yake kutoka makao ya wanajeshi hao.
Rais Maduro alionekana kuonyesha ujasiri mkubwa licha ya shtuma kutoka kwa Bw Guaido na jamii ya kimataifa, alipoungana na wanajeshi hao kuomboleza vifo vya wanajeshi saba kwenye ajali ya helikopta wiki jana.
Kupitia akaunti yake ya Twitter, Bw Guaido naye aliwaomba raia kutoka kila pembe ya nchi kuandaa maandamano hadi kambi ya kijeshi iliyoko karibu nao ili kuwashawishi wanajeshi wasiendelee kuunga mkono serikali ya Rais Maduro.
“Lengo letu ni kuwasilisha ujumbe wetu bila kuvurugana na jeshi na kusababisha umwagikaji wa damu,” akasema Bw Guaido.?Uhasama kati ya viongozi hao wakuu mara kadhaa umesabibisha mtafaruku na mapigano kati ya walinda usalama na waandamanaji.