'Virusi vya corona vyapatikana katika manii'
CHARLES WASONGA na MASHIRIKA
WATAFITI nchini China wamepata virusi vya corona ndani ya manii ya idadi fulani ya wanaume walioambukizwa ugonjwa wa Covid-19.
Hali hii imeibua hofu kuwa huenda kuna uwezekano wa virusi hivyo kusambazwa kimapenzi.
Uchunguzi huo uliendeshwa na madaktari katika Hospitali ya Manispaa ya Shangqiu katika wanaume 38 waliolazwa humo wakiugua Covid-19.
Ilibainika kuwa sita kati yao walikuwa na virusi vya corona katika manii yao.
Watafiti hao wanasema kuwa kwa kuwa matokeo hayo yalipatikana kutokana na uchunguzi uliofanywa kwa idadi ndogo ya wanaume, tafiti zingine zinafaa kufanywa kubaini ikiwa virusi hivyo vinaweza kupitishwa kupitia ngono.
“Tafiti zaidi zinafaa kufanywa kubaini ikiwa virusi vya corona vinaweza kuishi ndani ya manii,” watafiti hao waliandika katika Jarida ya Chama cha Matabibu wa Amerika (AMA).
“Ikiwa itathibitishwa kuwa virusi vya corona vinaweza kupitishwa kupitia tendo la ndoa hali hii inaweza kutoa habari muhimu kuhusu njia za kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo,” wakasema.
Hata hivyo, wataalamu wengine wanaelezea matokeo hayo kama mageni lakini hayapaswi kuaminika zaidi kwa sababu ni idadi ndogo ya watu waliohusishwa katika uchunguzi huo.
Uchunguzi wa awali uliofanywa nchini China katika miezi Fabruari na Machi ulibaini kuwa wagonjwa 12 waliochunguzwa hawakupatikana na virusi vya corona katika manii yao.
Allen Pacey, Profesa katika Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza alisema matokeo ya utafiti huo hayafai kuaminiwa zaidi.
“Hii ni kwa sababu utaratibu wa kuchunguza manii kwa ajili ya kubaini virusi vya corona ni mchakato wenye changamoto nyingi. Na uwepo wa virusi hivyo katika manii haukuonyesha ikiwa vilikuwa hai na vyenye uwezo wa kusababisha maambukizi,” akaeleza.
Lakini akaonya: “Hata hivyo, tusishangae ikiwa virusi vinavyosababisha Covid-19 vinaweza kupatikana ndani ya manii ya baadhi ya wanaume, kwani hali kama hii imebainika kuhusiana na virusi vinavyosababisha magonjwa mengine kama vile Ebola na Zika.”
Hata hivyo, Shirika la Afya Ulimwengu (WHO) linashikilia kuwa njia iliyothibitishwa ya kusambaa kwa virusi vya corona ni unyevunyevu unaoachiliwa hewani baada ya mgonjwa kukohoa au kupiga chafya.