KimataifaMakala

Waamerika wengi walivyofikiria kuhama US baada ya kuona Trump akimbwaga Kamala

Na MASHIRIKA November 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UCHAGUZI wa Amerika (US) ulipoashiria Donald Trump ataingia Ikulu ya Whitehouse kwa muhula wa pili, Waamerika wengi walianza kuchukua hatua nyingine: kuenda ughaibuni.

Takwimu za utafutaji maelezo katika mtandao wa Google zilionyesha kuwa Waamerika walikuwa wameandika “Move to Canada (Kuhamia Canada).

Baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa mnamo Jumanne eneo la Pwani Mashariki ya Amerika, utafutaji huu ulipanda kwa asilimia 1,270 ndani ya saa 24.

Utafutaji sawia kuhusu kuhamia New Zealand uliongezeka kwa takriban asilimia 2,000 huku ule wa Australia ukipanda kwa asilimia 820.

Ulipofika Jumatano jioni katika Pwani Mashariki ya US, utafutaji wa maelezo ya kuhama katika mtandao wa Google ulipanda kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa nchi hizo tatu. Haya ni kwa mujibu wa afisa mmoja wa Google.

Kampuni hiyo haijatoa takwimu kamili ya utafutaji huu.

Kwa mujibu wa maelezo katika tovuti ya Uhamiaji nchini New Zealand, tovuti hiyo ilionyesha watumiaji wapya angalau 25,000 kutoka Amerika waliingia katika tovuti hiyo ikilinganishwa na 1,500 wakati sawia mwaka uliopita.

Baadhi ya mawakili wa masuala ya uhamiaji wanapokea maswali mengi.

“Kila baada ya dakika 30 kuna barua pepe mpya,” alisema Bw Evan Green, mshirika mwenza katika kampuni kongwe zaidi ya uwakili nchini Canada – Green and Spiegel.

Hamu ya ghafla ya kuhama inaenda sawa na matamanio ya kuhamia ughaibuni yaliyoonekana Trump aliposhinda uchaguzi wa 2016.

Lakini wakati huu, kuchaguliwa tena kwa chama cha Republican kulijiri baada ya takriban wapigakura 75 kuhisi demokrasia ya Amerika ilikuwa katika hatari. Hii ni kulingana na Shirika la Utafiti la Edison.

 Vile vile, Waamerika wengi wana wasiwasi kuwa urais wa Trump utazidisha mgogoro kati ya Democrats na Republicans kuhusiana na rangi, jinsia, wanachofunzwa watoto shuleni na haki za masuala ya kizazi.

“Hii inasababishwa na Trump, lakini pia ni hali ya kijamii. Wengi wa Waamerika walimpigia kura na baadhi ya watu hawana furaha kuishi katika jamii ya aina hii tena. Watu wana hofu kuwa watapoteza uhuru wao,” alisema Bw Green.

Katika kundi la mtandao wa Reddit la watu wanaohama Amerika kwa jina “r/AmerExit,” mamia walipendekeza sehemu bora za kuhamia na njia za kupata visa na ajira.

Baadhi yao walisema wanahofia nchi yao, usalama wao, ama zote mbili baada ya Trump kuchaguliwa.

Hata kabla ya uchaguzi, wasiwasi huo uliongezeka miongoni mwa Waamerika ambao walikuwa na nia ya kuhamia Canada, haya ni kulingana na Bi Heather Bell ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uhamiaji katika kampuni ya uwakili ya Bell Alliance huko Vancouver.

“Hata hivyo, ni wachache walifaulu,” alisema Bi Bell. “Kuhamia Canada si rahisi, hasaa wakati huu ambapo serikali inapunguza idadi ya wanaohamia Canada kwa muda mfupi ama wa kudumu.”