Kimataifa

Waandamanaji sasa wapiga kambi katika makao ya wanajeshi

April 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

VIKOSI vya usalama Jumatatu vililazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya maelfu ya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum, kumshinikiza Rais Omar el Bashir kuondoka uongozini.

Waandamanaji hao wanamtaka Bashir wanamlaumu Bashir kutokana na hali mbaya ya uchumi wa taifa hilo.

Vilevile, wanamlaumu kwa kuongezeka kwa bei za bidhaa za msingi kama vile mkate.

Mnamo Februari, Bashir alitangaza hali ya hatari nchini humo, akisema kuwa hatakubali watu wachache wavuruge udhabiti wa taifa hilo.

Watu ambao hawakutaka kutajwa walisema vikosi vya ujsalama viliziba barabara zinazoelekea katika makao yake makuu.

“Waliziba barabara zote kwa kutumia vifaru na walikuwa wamejihami vikali,” akasema mwandamanaji mmoja.

Ripoti zilieleza kuwa gesi hiyo iliwaathiri watu walio umbali wa hadi kilomita tano kutoka eneo la maandamano.

“Nilitoka nje ya nyumba yangu baada ya kusikia mlio mkubwa wa gesi ikirushiwa waandamanaji,” akasema mkazi mmoja.

Waandamanaji hao wanalishinikiza jeshi kuwaunga mkono kwenye rai zao kumtaka Rais Bashir kuondoka mamlakani.

Wamekuwa wakiendeleza maandamano kupitia kauli: “Sudan imeamka ! Jeshi limeamka!”

Makao makuu ya jeshi yanapakana na makazi ya kiongozi huyo.

Rais Bashir amekuwa uongozini kwa zaidi ya miongo mitatu.

Waandalizi wa maandamano hayo walichagua Jumamosi kama siku maalum ya kupiga kambi katika makao hayo, ili kuwiana na mengine yaliyomwondoa mamlakani rais wa zamani Jaafar Numeiri mnamo 1985.

Licha ya shinikizo zinazomkabili, Rais Bashir amekataa kung’atuka, akishikilia kuwa wapinzani wake wanalenga kumwondoa uongozini kwa njia ya mkato. Anasema kuwa atakubali tu kuondoka ikiwa atashindwa katika uchaguzi.

Vifo

Makundi ya kutetea haki za binadamu yanashikilia kuwa watu 51 ndiyo wameuawa tangu maandamano hayo kuanza mnano Jumamosi.

Yanadai watu hao wameuawa na vikosi hivyo, yakiyalaumu kwa kuwafyatulia risasi.

Mwandamanaji mwingine aliuawa katika maandamano tofauti katika mji wa Omdurman, ulio wa pili kwa ukubwa.

Kijumla, serikali inashikilia kuwa watu 32 ndiyo wameuawa tangu maandamano kuanza mnamo Desemba, huku shirika la Human Rights Watch likisema ni watu 51 waliouuawa.

Mamia ya watu ambao wamekuwa wakishiriki katika maandamano hayo wamekamatwa na wanaendelea kuzuiliwa na serikali hiyo.

Miongoni mwao ni viongozi wa vyama vya upinzani, wanaharakati na waandishi wa habari.

Shirika la Kitaifa la Kijasusi nchini Sudan ndilo linalolaumiwa kwa kuwakamata watu hao.