Waasi watangaza mwisho wa utawala wa Rais Assad nchini Syria, duru zikisema ametorokea kusikojulikana
WAASI wa Syria walisema Jumapili kwamba wamemaliza utawala wa kimabavu wa miaka 24 wa Bashar al-Assad, katika tangazo lao la kwanza kwenye televisheni ya taifa kufuatia shambulio ambalo liliishangaza dunia.
Jeshi la Syria liliwaarifu maafisa Jumapili kwamba utawala wa Assad umeisha, afisa wa Syria ambaye alifahamishwa kuhusu hatua hiyo aliambia Reuters.
Lakini jeshi la Syria baadaye lilisema lilikuwa likiendelea na operesheni dhidi ya “makundi ya kigaidi” katika miji muhimu ya Hama na Homs na eneo la mashambani la Deraa.
Assad, ambaye alikuwa amezima aina zote za upinzani, aliondoka Damascus na kuelekea kusikojulikana mapema Jumapili, maafisa wawili wakuu wa jeshi waliambia Reuters, huku waasi wakisema kuwa wameingia katika mji mkuu bila dalili ya kukabiliwa na jeshi.
“Tunasherehekea pamoja na watu wa Syria habari za kuwaachilia wafungwa wetu na kuachilia minyororo yao na kutangaza mwisho wa enzi ya ukosefu wa haki katika gereza la Sednaya,” waasi walisema, wakimaanisha gereza kubwa la kijeshi nje kidogo ya Damascus ambapo serikali ya Syria iliwazuilia maelfu.
Maelfu ya watu wakiwa kwa magari na kwa miguu walikusanyika katika uwanja mkuu huko Damascus wakipunga mkono na kuimba “Uhuru” kutoka kwa nusu karne ya utawala wa familia ya Assad, walioshuhudia walisema.
Kuporomoka kwa Assad kunaashiria wakati wa mabadiliko Mashariki ya Kati, na kumaliza utawala wa kidikteta wa familia hiyo Syria na kusababisha pigo kubwa kwa Urusi na Iran, ambazo zimepoteza mshirika mkuu eneo hilo.
Kasi ya matukio imeishangaza miji mikuu ya Kiarabu na kuibua hofu ya wimbi jipya la ukosefu wa utulivu wa kikanda.
Inaashiria hatua ya mabadiliko kwa Syria, iliyopondwa na vita vya zaidi ya miaka 13 ambavyo vimegeuza miji kuwa vifusi, kuua mamia ya maelfu ya watu, na kuwalazimisha mamilioni nje ya nchi kama wakimbizi.
Kuimarisha maeneo ya magharibi mwa Syria yaliyotekwa waasi itakuwa muhimu. Serikali za Magharibi, ambazo zimekwepa serikali inayoongozwa na Assad kwa miaka mingi, lazima ziamue jinsi ya kukabiliana na utawala mpya ambapo kundi la kigaidi – Hayat Tahrir al-Sham (HTS) – linaonekana kuwa na ushawishi.