Kimataifa

Wabunge wakerwa kupimiwa samaki mkahawani

June 20th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

DODOMA, TANZANIA

Na THE CITIZEN

WABUNGE wamekasirishwa na hatua ya serikali kuu kupima samaki wanaopakuliwa katika mkahawa wa bungeni.

Spika wa bunge, Dkt Tulia Ackson, aliagiza serikali kuu itoe taarifa rasmi kueleza jinsi maafisa wa Wizara ya Ustawishaji wa Mifugo Uvuvi walivyofanikiwa kuingia hadi bungeni kupima ukubwa wa samaki mkahawani.

“Kutokana na kuwa Waziri Mkuu yuko hapa, ninaagiza kwamba serikali ilete taarifa kamili hapa kuhusu suala hili ili tuarifiwe nini kilifanyika ndipo tuamue hatua tutakayochukua,” akasema.

Suala hilo liliibuka katika vikao vya bunge Jumanne jioni wakati Mbunge wa Kigoma Kaskazini Peter Serukamba alipoinuka kuomba bunge lilijadili.

“Hali ya kwamba maafisa walifanikiwa kuingia bungeni wakaenda moja kwa moja hadi sehemu ambapo chakula chetu huandaliwa inamaanisha usalama wetu pia unaweza kuwa hatarini. Wangewezaje kufanya hivyo bila kufahamisha afisi ya spika?” akauliza Bw Serukamba.

Hoja hiyo ilivutia wabunge wote kumi ambao walilijadili, huku wengine wakiuliza kama maafisa hao hufanya hivyo pia kwa asasi zingine za serikali ikiwemo afisi ya rais na mahakama.

-Imekusanywa na Valentine Obara