Wadadisi waonya ghasia zitachafua Tanzania
Na MASHIRIKA
MAAFISA wa usalama wa Tanzania wanashinikizwa wawaadhibu wanaotekeleza ghasia za kisiasa wakati huu wa kampeni huku wadau wakionya zinaweza kuharibu uchaguzi mkuu katika nchi hiyo unaopangwa kufanyika Oktoba 28. Wadadisi wanaonya visipokomeshwa vitachafua sifa za Tanzania.
Kumekuwa na madai ya wakora wa kukodishwa na maafisa wa polisi wenyewe kuhusika katika ghasia na Inspekta Jenerali wa polisi Simon Sirro wiki hii aliagiza uchuguzi kuhusu madai kwamba mgombeaji wa kiti cha ubunge cha Serengeti wa chama cha Chadema , Catherine Ruge, alishambuliwa na maafisa wa polisi.
Sirro aliambia wawakilishi wa vyama vya kisiasa kutoka Butiama, Serengeti, Musoma na Bunda kwamba maafisa wake watachukulia madai hayo kwa uzito lakini pia akawataka wanasiasa kuwajibika.
“Tutachunguza haya lakini kwa upande mwingine, viongozi wa kisiasa na wafuasi wao ni lazima watii sheria wakiendeleza shughuli zao,” alisema.
Bi Ruge alilalamika kuwa alidhulumiwa kimapenzi alipotembelea ofisi za afisa wa uchaguzi kufuatilia ombi la kutaka ratiba ya kampeni zake ibadilishwe aweze kutafuta matibabu.
“Afisa wa polisi alinishambulia. Walirarua mavazi yangu wakati wa kisa hicho,” alisema Ruge ambaye alitaja afisa huyo alipokutana na Sirro.
Alisema alienda katika ofisi za mkuu wa uchaguzi barua aliyoandika ilipokosa kujibiwa.
“Mnamo Oktoba 8 mwaka huu, viongozi wa Chadema walifuatilia barua hiyo lakini hawakupatiwa jibu. Hii ndio sababu niliamua kwenda huko binafsi. Nilipokuwa nikiketi ofisini, nilishambuliwa na polisi walionizuia. Baadaye waliniachilia kwa dhamana,” alisema.
Visa vya ghasia zimeongezeka sehemu za Tanzania uchaguzi ukikaribia.
Kanda za video zimekuwa zikisambazwa kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha mali ya mgombeaji wa chama cha Chadema eneobunge la Chato na afisa cha chama hicho ikichomwa.
Mkuu wa polisi eneo la Geita Sikoki Mwaibambe alithibitisha visa hivyo akisema kundi la kati ya wanaume saba na kumi walivamia boma la mgombeaji wa chama cha Chadema, wakaharibu ua na kuchoma kibanda alichokuwa ameegesha pikipiki yake.
Alisema polisi wanaendelea kuchunguza kisa hicho. Chadema ilitoa taarifa kuvikashifu vitendo vya ghasia dhidi ya mgombeaji wake na afisa wake.
Taarifa ilisema kwamba vitendo hivyo ni tishio kwa usalama wa wagombeaji na maafisa wake.
“Chadema inachukulia kisa cha Chato na vingine vilivyotokea Kahama kama tishio kwa mgombea urais Tundu Lissu. Tunachukulia hii kama ishara ya kuvuruga uchaguzi mkuu,” ilisema taarifa ya chama hicho.
Queen Sendiga, mgombea urais wa chama cha ADC, alisema vitendo hivyo vinapangwa na vyama vya kisiasa na wagombeaji ambao hawana ajenda ya kushawishi Watanzania. Kulingana na Dkt Paul Luisulie, mhadhiri katika chuo kikuu cha Dodoma, vitendo hivyo vitachafua sifa za Tanzania iwapo havitakomeshwa.