Kimataifa

Wafungwa 400 watoroka jela

September 3rd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA NA PETER MBURU

TRIPOLI, LIBYA

Wafungwa 400 walihepa kutoka gereza moja katika Jiji kuu la Libya, Tripoli baada ya maandamano ya fujo kutokea na kutawala jiji hilo wiki nzima.

Polisi wa Libya walisema wafungwa hao walivunja milango ya jela na kutoka, wakati vurugu baina ya polisi wa kukabiliana na ghasia zilifika karibu na gereza hilo la Ain Zara.

“Wafungwa waliweza kufungua milango kwa nguvu na kutoka,” idara ya polisi nchi hiyo ikasema.

Hata hivyo, polisi hawakusema makossa waliyokuwa wametenda wafungwa waliotoroka.

Habari ya polisi ilisema walinzi waliokuwa wakilinda doria walihofia maisha yao na kutoroka, baada ya kuona wafungwa wakitoka kwa nguvu.

Hata hivyo, ilibainika kuwa wengi wa wafungwa waliokuwa jela hiyo ni wale wa makossa ya kawaida ama waliokuwa wafuasi wa Rais wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi na waliopatikana na hatia ya kuua wakati wa fujo zilizotokea 2011.

Jiji kuu la Libya limezongwa na vita baina ya serikali ya sasa na vikundi vya waasi tangu kuuawa kwa Muammar Gaddafi, huku wizara ya afya ikiripoti kuwa angalau watu 39 wameuawa na 100 kujeruhiwa.