Walimu wapinga pendekezo Kiswahili kufunzwa shuleni Namibia
Na MASHIRIKA
BARAZA la Mawaziri la Namibia limeidhinisha hoja ya kutaka lugha ya Kiswahili ifundishwe shuleni.
Walimu hata hivyo, wamepinga hatua hiyo ya Baraza la Mawaziri huku wakisema kuwa Kiswahili kitachanganya wanafunzi, kulingana na gazeti la The Namibian.
Hoja hiyo ilipitishwa na Baraza la Mawaziri wiki iliyopita.
Serikali ya Namibia ilianza kujadili suala la kufundisha lugha ya Kiswahili baada ya kiongozi wa Tanzania John Magufuli kuzuru nchi hiyo Mei, mwaka huu.
Wakati wa ziara yake, Rais Magufuli alitaka Namibia na Tanzania kudumisha ushirikiano ambao umekuwepo tangu 1991 kwa kufundisha Kiswahili.
Magufuli alisisitiza kuwa kulikuwa na haja kwa mataifa hayo mawili kushirikiana katika sekta ya elimu.
“Tunatarajia kuwa Namibia itafuata nyayo za mataifa yaliyo katika Muungano wa Maendeleo wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kujumuisha Kiswahili katika mtaala wake wa elimu. Nchi nyingine za SADC kama vile Rwanda na Afrika Kusini zimeanza kufundisha Kiswahili. Tanzania itatoa walimu na vifaa vya kufundishia,” akasema Rais Magufuli.
Kiswahili huzungumzwa katika mataifa 14 barani Afrika lakini kimetia fora nchini Tanzania, Kenya na Uganda.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu nchini Namibia, Mahongora Kavihuha alisema kuwa hawatapinga kufundishwa kwa lugha ya kigeni ili mradi iwafae wanafunzi.
“Ikiwa lugha hiyo mpya itasaidia kuboresha maisha ya wanafunzi na hata kuwaongezea uwezekano wa kupata ajira hatupingi,” akasema.
Kavihuha hata hivyo, alionya kuwa uamuzi huo wa serikali unafaa kutathminiwa kwa uangalifu kabla ya kuanza kufundisha Kiswahili.
“Serikali inafaa kutueleza manufaa ambayo wanafunzi watapata kwa kufundishwa Kiswahili,” akasema.
Mkuu wa Kitivo cha Lugha na Fasihi katika Chuo Kikuu cha Namibia, Jekura Kavari, alipinga hoja hiyo ya kutaka Kiswahili kufundishwa.
Kavari alisema serikali ya Namibia inafaa kutoa fursa ya lugha za mama nchini humo kukua kabla ya kuanza kufundisha lugha ya kigeni.
“Serikali imekuwa ikisema kuwa haina fedha za kukuza lugha zetu humu nchini kufikia kiwango cha kimataifa. Watatoa wapi fedha za kufunzia Kiswahili?” akauliza. Kavari alisema lugha ya Kiswahili ina asili ya Kibantu sawa na lugha nyingi za kiasili zinazozungumzwa nchini Namibia hivyo huenda ikachanganya wanafunzi.
“Ikiwa lugha inakaribiana na yako unayozungumza kila siku inaweza kukukanganya,” akasema.