Wamaasai wapigwa marufuku kutembea na visu vya kitamaduni visiwani Zanzibar
NA CHARLES WASONGA
SERIKALI ya Zanzibar imepiga marufuku mtindo wa watu wa jamii ya Maasai kutembea hadharini wakiwa wamebeba silaha za kitamaduni.
Kulingana na mtandao wa habari wa SwahiliTimes, serikali hiyo ilisema marufuku hayo yalitolewa kwa msingi kuwa utamaduni huo unahatarisha maisha ya watu na ni unaenda kinyume na tamaduni za visiwa vya Zanzibar.
Hatua hiyo imejiri baada ya video moja kusambaa mitandaoni ikiwaonyesha watu wa jamii ya Kimaasai wakimshambulia afisa mmoja wa Idara ya Kudhibiti Silaha za Jadi alipokuwa akihakikisha utekelezaji wa sheria zinazozuia uendeshaji wa biashara ndogondogo kando mwa barabara za mji wa Mkongwe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mjini Rashid Msaraka alisema sheria na kanuni za Zanzibar haziruhusu watu kutembea hadharani wakibeba silaha za kitamaduni.
“Watu wanahimizwa kuacha marungu na visu vya kitamaduni au sime nyumbani. Wasitembee na silaha hizi kwa sababu hapa sio msituni na hamna wanyama wakali wanaohatarisha maisha ya watu. Kwa hivyo watu wa jamii ya Kimaasai wanapaswa kutii sheria, kanuni na tamaduni za kisiwa cha Zanzibar,” akaeleza.
Watu wa jamii ya Wamaasai wanaoishi Kenya na Tanzania hutembea wakibeba fimbo inayokulikana kwa Kimaasai kama “eng’udi”, rungu, sime au upanga (olalem), mkuki (eng’erempe au empere), silaha ambazo wao huwa hawatumii kupigana na mtu.
Kulingana na mwandishi wa riwaya marehemu Henry Ole Kulet, silaha hizo huwa ni sehemu ya mavazi ya watu wa jamii ya Wamaasai.
“Serikali inatambua hizo kama sehemu ya mavazi yetu ya kitamaduni na ndio maana Mmaasai hawezi kukamatwa na walinda usalama anapotembea na silaha hizo,” anasema katika mojawapo ya machapisho yake.
Kipengele cha 11 cha Katiba ya sasa kinatambua mila na tamaduni kama msingi wa taifa la Kenya.
Kwa hivyo ni wajibu wa serikali: “Kuendeleza aina zote za tamaduni za jamii za Kenya zinazodhihirishwa kwa njia za sanaa, mavazi, fasihi, michoro, vinyago miongoni mwa njia nyingine.”