Wanafunzi 25 wathibitishwa kufariki baada ya ndege ya kijeshi kuangukia shule
DHAKA, BANGLADESH
ZAIDI ya wanafunzi 25 walikuwa kati ya watu 27 ambao walikufa na kuondolewa kwenye jengo lililoteketezwa baada ya ndege ya jeshi la angani la Bangladesh kupata ajali Jumatatu jijini Dhaka.
Ndege hiyo iliyokuwa ikitumika kwa mafunzo ya kijeshi, ilianguka kwenye jengo la shule na taasisi ya mafunzo.
Mbali na maafa hayo ya kusikitisha, watu 88 na wamelazwa hospitalini wakipokea matibabu.
Ikiwa aina ya F-7 BGI, ilianguka baada ya kupaa angani saa saba na dakika sita mchana kutoka kwa makao ya jeshi la angani, Kurmitola.
Jeshi lilitoa taarifa na kusema ajali hiyo ilitokana na tatizo la kiufundi.
Picha zilionyesha waokoaji wakiondoa vifusi kwenye jengo ambalo lilichomeka moto baada ya kuangukiwa na ndege hiyo.
Wanafamilia ambao jamaa zao walikufa na wengine kujeruhiwa nao walionekana kujawa na huzuni isiyopimika.
Seyedur Rahman, mshauri wa masuala ya afya alithibitisha kuwa watu 27 walikuwa wamekufa na wengine 88 walikuwa wakipokea matibabu hospitalini.
Waliokufa ni watoto 25, mwalimu na rubani kwa mujibu wa Rahman.
Kutokana na mauti na majeraha hayo, serikali ilitangaza siku ya maombolezo, bendera zikipeperushwa nusu mlingoti na kuandaliwa kwa maombi maeneo yote ya ibada.
F-7 BGI ni ndege ya kisasa yenye teknolojia ya juu kutoka kampuni ya kutengeneza ndege aina ya J-7/F-7.
Bangladesh ilitia saini mkataba wa kununua ndege 16 za f-7 BGI mnamo 2011 na zikawasilishwa zote kufikia mnamo 2011.
Ajali hiyo inatokea wakati ambapo India, jirani ya Bangladesh bado ina makovu ya ajali mbaya zaidi ya ndege mwezi uliopita.
Kwenye kisa cha India, ndege ya jeshi la angani iliangukia taasisi ya mafunzo ya kimatibabu mjini Ahmedabad na kuwaua abiria 241 kati ya 242 waliokuwa ndani.
Watu wengine 19 nao walikufa baada ya kuangukiwa na ndege hiyo ardhini.