Wanafunzi wajawazito sasa kuenda shuleni bila vikwazo
Na MASHIRIKA
HARARE, Zimbabwe
RAIS wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametia sahihi sheria inayozuia shule za umma kuwatenga wasichana wanaopachikwa mimba dhidi ya kuhudhuria masomo.
Walimu hawakubaliwi tena kuwachapa watoto kupitia marekebisho hayo ya Mswada kuhusu Elimu ambao ulipitishwa kuwa sheria mnamo Jumamosi.
Aidha, sheria hiyo inasema kuwa hakuna mwanafunzi atakayezuiwa kwenda shule kwa kukosa karo.
Kabla ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho, usimamizi wa shule ungemfukuza msichana kwa kutungwa mimba huku ukimruhusu mvulana aliyehusika na ujauzito huo kuendelea na masomo, jambo lililoonekana kama ubaguzi dhidi ya mtoto wa kike.
Wataalam wa elimu walikaribisha marekebisho hayo huku Waziri wa Elimu ya Shule ya Msingi na Shule ya Upili Cain Mathem, akisema kuwa alijawa na furaha kufuatia hatua ya rais kuidhinisha sheria hiyo mpya.
“Rais ametia sahihi sheria hiyo na tutatekeleza kikamilifu vipengele hivyo ili kuendeleza elimu nchini. Tunaamini kuwa sheria hiyo ni uamuzi unaoweza kuendelezwa,” alisema.
Mkurugenzi wa Muungano wa Elimu Zimbabwe (Zimta) Sifiso Ndlovu, alisema wanaunga mkono vipengele vya sheria hiyo kwa kuwa vinaambatana na jamii ya kisasa.
Alisema adhabu ya kiboko inaunda jamii katili na kwamba ni vyema ilifutiliwa mbali huku sheria ya kuruhusu masomo kwa wanafunzi wajawazito ikisaidia kuendeleza haki za mtoto wa kike.
“Kama Zimta, tulihusika kikamilifu kubuni sheria hiyo. Sehemu kubwa ya vipengele tulivyopendekeza vimejumuishwa. Tunapinga adhabu ya kiboko kwa sababu ni mtindo uliopitwa na wakat wa kudumisha nidhamu. Matokeo yake ni kuwa na jamii katili.
“Tunaunga mkono pia mikakati yoyote inayodhamiriwa kulinda maslahi na haki za mtoto msichana. Mojawapo wa sheria hizo ni kupiga marufuku hatua ya kuwatenga wanaoshika mimba. Jambo hili limekuwa likizingatiwa na jamii nyinginezo na tunaunga mkono kabisa kipengele hicho,” alisema Ndlovu.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Walimu kuhusu Uendelezaji, Raymond Majongwe alisema huku sheria ikilinda haki za wasichana, kuna hofu kwamba baadhi ya watu watatumia vibaya fursa hiyo kujinufaisha.
Alisema kunapaswa kuwepo majadiliano zaidi kuhusu suala la adhabu ya kiboko kwa sababu wanafunzi huenda wakajihusisha na utovu wa nidhamu wakijua kwamba hawawezi kuadhibiwa.